Aug 02, 2020 11:27 UTC
  • Alexander Grushko
    Alexander Grushko

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametahadharisha kuhusu uwezekano wa dunia kurejea katika kipindi cha Vita Baridi.

 Alexander Grushko amesema kuwa, jitihada inazofanyika kwa ajili ya kuwa na nguvu kubwa za kijeshi katika eneo la mashariki mwa Ulaya ni sera haribifu ambayo inaifanya hali ya sasa kuwa sawa na ile ya kipindi cha Vita Baridi.

 Grushko amesisitiza kuwa, ushindani unaoshuhudiwa baina ya nchi za Ulaya Mashariki kwa ajili ya kuwa mwenyeji wa vikosi vya majeshi ya Marekani hauimarishi usalama wa nchi hizo. Ameongeza kuwa, hatua hiyo haiheshimu maslahi ya nchi zote za eneo la Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amezitaka nchi za Ulaya Mashariki kutupilia mbali mashindano ya kutaka kuwa mwenyeji wa vikosi vya majeshi ya Marekani akisisitiza kuwa maafikiano na Marekani hayawezi kudumu. 

 Alexander Grushko amesema kuwa, usalama wa Ulaya hauwezi kudhaminiwa bila ya kuishirikisha Russia.

Mipango inayofanywa na Rais Donald Trump wa Marekani na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya nchi hiyo ya kupeleka vikosi vya majeshi ya Marekani katika nchi za Ulaya Mashariki imekabiliwa na upinzani mkubwa wa serikali ya Russia. 

Tags

Maoni