Aug 04, 2020 03:33 UTC
  • Abe Shinzo: Mashambulio ya atomiki ya Hiroshima na Nagasaki hayapasi kurudiwa tena

Waziri Mkuu wa Japan amesisitiza kuwa mashambulio ya mabomu ya atomiki yaliyofanywa dhidi ya miji ya nchi hiyo ya Hiroshima na Nagasaki hayapasi kurudiwa tena.

Abe Shinzo ametoa sisitizo hilo sambamba na kukaribia maadhimisho ya mwaka wa 75 tangu miji hiyo iliposhambuliwa na Marekani kwa kutumia mabomu hayo angamizi.

Mbali na kuzipa mkono wa pole familia za waathirika wa mashambulio ya Marekani katika miji ya Hiroshima na Nagasaki, Abe Shinzo amesisitiza kuhusu ahadi iliyotoa nchi yake kuhusiana na misingi mitatu ya kutounda, kutoziweka na kutoziingiza nchini Japan silaha za atomiki.

Waziri Mkuu wa Japan anatazamiwa kushiriki katika maadhimisho ya tukio hilo yatakayofanyika siku ya Alkhamisi.

Tarehe 6 Agosti 1945, ndege moja ya kivita ya jeshi la Marekani aina ya B-29 ilidondosha bomu la atomiki katika mji wa Hiroshima nchini Japan kwa amri ya rais wa wakati huo wa Marekani Harry Truman.

Hali ya kusikitisha ya mmoja wa manusura wa mashambulio ya atomiki ya Marekani dhidi ya miji ya Japan

Siku tatu baadaye, Marekani iliwadondoshea bomu jengine la atomiki raia wa Japan wa mji wa Nagasaki.

Watu wapatao 220,000 walipoteza maisha kutokana na mashambulio hayo mawili yaliyofanywa na Marekani.

Mashambulio ya silaha za nyuklia dhidi ya miji ya Hiroshima na Nagasaki ndio matukio pekee ya utumiaji wa silaha hizo angamizi kuwahi kufanywa vitani duniani hadi sasa.

Pamoja na hayo, Marekani haijawahi wakati wowote ule kuomba radhi kwa kutumia mabomu hayo kuwashambulia na kuwaua raia wa miji hiyo miwili ya Japan.../

Maoni