Aug 04, 2020 08:03 UTC
  • Juan Carlos
    Juan Carlos

Mfalme wa zamani wa Uhispania, Juan Carlos ameondoka nchini humo na kuelekea kusikojulikana wiki kadhaa baada ya kuhusishwa na ufisadi na kashfa ya kupokea mlungula kutoka kwa mfalme wa zamani wa Saudi Arabia.

Juan Carlos, 82, alitangaza hatua hiyo jana Jumatatu katika barua aliyomwandikia mtoto wake, Felipe, ambaye alimkabidhi madaraka miaka sita iliyopita.

Mwezi Juni mwaka huu Mahakama Kuu ya Uhispania ilifungua uchunguzi kuhusu madai ya kuhusika Juan Carlos katika mkataba wa ujenzi wa reli ya kasi kubwa inayounganisha miji ya Makka na Madina nchini Saudi Arabia.

Baadhi ya vyombo vya habari vinasema mfalme huyo wa zamani wa Uhispania ameelekea katika Jamhuri ya Dominican.

Kuondoka kwa namna hii kwa Juan Carlos kumetambuliwa kuwa ni kwa madhila kwa kiongozi ambaye hapo awali alionekana kuwa ameweka historia kama mtu ambaye aliongoza Uhispania kwa ustadi kutoka utawala wa kidikteta hadi demokrasia baada ya kifo cha Jenerali Franco mnamo 1975.

Gazeti la La Tribune de Genève la Uswisi lilifichua kuwa mfalme huyo wa zamani wa Uhispania alipokea mlungula wa dola milioni 100 kutoka kwa mfalme wa zamani wa Saudi Arabia.

Juan Carlos na mfalme wa zamani wa Saudia Abdullah bin Abdul Aziz

Wafalme wa Uhispania wana kinga ya kufikishwa mahakamani wanapokuwa madarakani lakini Juan Carlos alijiengua na kukabidhi madaraka kwa mwanaye, Felipe mwaka 2016; hivyo anaweza kupandishwa kizimbani.

Tags

Maoni