Aug 04, 2020 11:13 UTC
  • Wananchi wa Ujerumani waunga mkono kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini mwao

Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa Ujerumani unaonyesha kuwa akthari ya raia wa nchi huo wanaunga mkono kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini mwao na pia wanataka Marekani iondoe silaha zake za atomiki katika ardhi ya nchi hiyo.

Uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na Taasisi ya YouGov umeonyesha kuwa asilimia 66 ya wananchi wa Ujerumani wanaunga mkono mpango wa kuondoa nchini humo silaha za nyuklia za Marekani na ni asilimia 19 tu wanaotaka silaha hizo za Marekani zisalie nchini humo. 

Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi huo wa maoni ya Taasisi ya YouGov, karibu robo ya wananchi wa Ujerumani wanaamini kuwa  vikosi vya usalama vya Marekani vinapasa kuondoka kikamilifu katika ardhi ya Ujerumani. 

Marekani ina mpango wa kuzihamishia nchini Italia ndege zake za kivita aina ya F-16; ambazo sasa zipo katika jimbo la Rhineland-Palatinate huko Ujerumani. 

Wakati huo huo Mark Esper Waziri wa Ulinzi wa Marekani wiki iliyopita alitangaza kuwa ana mpango wa kuwaondoa Ujerumani wanajeshi wa Marekani karibu 12,000.  Kwa mujibu wa mpango huo, karibu wanajeshi 6,400 watarejea Marekani na wengine karibu 5,400 wanapelekwa katika nchi nyingine za Ulaya. 

Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani  

Rais Donald Trump wa Marekani ametishia mara nyingi kwamba ataondoa wanajeshi wa nchi hiyo waliopo Ujerumani kwa sababu serikali ya nchi hiyo imekataa kuongeza gharama za matumizi ya kijeshi.  

Tags

Maoni