Aug 05, 2020 06:02 UTC
  • Uchumi wa Marekani watumbukia katika mdororo mkubwa

Uchumi wa Marekani umeingia katika mdororo mkubwa kutokana na athari mbaya za maambukizi ya virusi vya corona. Uchunguzi wa taasisi ya ISM umebaini kuwa, katika kipindi cha miezi mitatu ya pili ya mwaka huu wa 2020 uchumi wa Marekani umeingia katika mdororo mkubwa zaidi wa kiuchumi ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo tangu wakati wa mdororo mkubwa wa mwa 2007 hadi 2009.

Uchumi mkuwa zaidi wa dunia umepungua kwa asilimia 9.5 katika kipindi cha miezi Aprili na Juni. Takwimu hizi zina maana kwamba, iwapo mwenendo wa uchumi wa Marekani utakuwa hivi hivi katika misimu mitatu ijayo basi thuluthi moja ya uchumi wa nchi hiyo itayeyuka na kuyoyoma kutokana na maambukizi ya virusi vya corona na taathira zake mbaya. Mdororo huu haujawahi kushuhudiwa nchini Marekani tangu kulipoanza kutolewa takwimu za ustawi wa uchumi wa kila msimu hapo mwaka 1947. 

Kabla ya mlipuko wa maambukizi ya corona kiwango cha chini zaidi cha uzalishaji ghafi wa ndani wa Marekani kilishuhudiwa katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 1958. Uzalishaji ghafi wa ndani wa Marekani wakati huo ulipungua kwa asilimia 10 kwa mwaka. Dhoruba ya kiuchumi iliyoikumba Marekani katika miezi mitatu ya pili ya mwaka huu ni kubwa zaidi mara nne ya mdororo mbaya zaidi wa kiuchumi wa msimu wa mwaka 2007 hadi 2009. Takwimu za Ofisi ya Utafiti wa Kiuchumi ya Marekani zinasema kuwa, shughuli za kiuchumi nchini humo zimepungua kwa asilimia 5 katika miezi mitatu ya mwanzoni mwa mwaka huu. Kupungua ustawi wa uchumi wa Marekani na kutumbukia katika mdororo kuna maana ya kuanza kufilisika makampuni makubwa na ongezeko kubwa la watu wasio na ajira. Katika mwezi Aprili mwaka huu peke yake Wamarekani zaidi ya milioni 20 walipoteza kazi na ajira zao. 

Uchumi wa Marekani waporomoka kwa asilimia 9.5 katika miezi ya Aprili na Juni 

Seneta wa jimbo la Vermont, Bernie Sanders amesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter kwamba: "Wananachi wa Marekani wamekuwa maskini zaidi." Sanders ametahadharisha kuwa, corona imezifanya nusu ya familia za Marekani pia zipoteze kipato chao. Amesema: "Matajiri wamezidisha utajiri wao lakini zaidi ya nusu ya familia za Wamarekani zimepoteza kipato chao katika kipindi hiki cha maambukizi ya corona... Tunahitaji uchumi utakaohudumia watu wote na si uchumi feki unaowanufaisha matajiri na wenye madaraka."

Seneta Bernie Sanders anasema kuwa, uzalishaji ghafi wa ndani wa Marekani pia umepungua kwa asilimia 33 katika miezi mitatu iliyopita. 

Athari mbaya na haribifu za mlipuko wa corona zimetoa changamoto kubwa kwa utawala wa Marekani katika masuala ya usimamizi wa masuala ya kifedha na kiuchumi. Ikulu ya rais wa nchi hiyo, White House inawalaumu Wademokrat wanaodhibiti Kongresi kwamba ndio sababu ya kutopatikana mwafaka wa muda mfupi kuhusiana na bima ya wasio na ajira na kusitishwa kasi ya kufukuzwa watu katika maeneo ya ajira na kazi. Hata hivyo Waripublican wenyewe ambao wamekwamisha mazungumzo rasmi ya kujadili kadhia ya kupasisha kifurushi cha kuhamasisha uchumi kwa kipindi cha wiki moja, bado hawajafikia mwafaka bina yao wenyewe.

Virusi vya corona vilivyoiathiri pakubwa Marekani  

Miongoni mwa athari mbaya za maambukizi ya virusi vya corona na kupungua ustawi wa kiuchumi wa Marekani ni kuongezeka ukosefu wa usawa na ufa mkubwa wa kiuchumi nchini humo. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, kama alivyoashiria Seneta Bernie Sanders, matajiri wanazidi kuwa matajiri na masikini wanadidimia zaidi katika dimbwi la umaskini nchini Marekani.

Televisheni ya Bloomberg imeripoti kuwa, ukosefu wa usalama wa chakula baina ya familia za Kimarekani umefikia kiwango chake cha juu zaidi na karibu Wamarekani milioni 30 hawakuwa na chakula cha kutosha katika siku 7 zilizoishia tarehe 21 mwezi Julai.

Ripoti ya Bloomberg imeongeza kuwa: Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Idara ya Takwimu ya Marekani baina ya familia za nchi hiyo umeonesha kuwa, takriban Wamaekani milioni 23 hawakuwa na chakula cha kutosha kwa kipindi cha wiki moja na zaidi ya wengine milioni tano hawakuwa na chochote cha kula katika wiki hii.

Hii ndiyo hali ya nchi inayodai kuwa dola kubwa zaidi duniani, nchi ambayo bajeti yake ya masuala ya kijeshi ni zaidi ya dola bilioni 700 lakini mamilioni ya raia wake wanashindwa kupata chakula cha kutosha.

Maoni