Aug 05, 2020 16:42 UTC
  • Katika kila sekunde 15 mtu mmoja anafariki dunia kwa maradhi ya Covid-19

Idadi ya vifo vinavyosababishwa na maradhi ya Covid-19 imepindukia 700,000 duniani kote huku Marekani, Brazil, India na Mexico zikiwa zinaongoza kwa ongezeko la idadi ya vifo.

Uchunguzi wa kitakwimu uliofanywa na shirika la habari la Reuters kulingana na makadirio ya kipindi cha majuma mawili yaliyopita unaonyesha kuwa, kwa wastani, karibu watu 5,900 huaga dunia kwa ugonjwa wa COVID-19 ndani ya muda wa saa 24. Idadi hiyo ni sawa na vifo 247 katika kipindi cha saa moja au kifo cha mtu mmoja katika muda wa sekunde 15.

Hayo yanaripotiwa huku Rais Donald Trump wa Marekani akidai kuwa mripuko wa virusi vya corona unaendelea kudhibitiwa nchini humo ambako watu zaidi ya 155,000 wameshapoteza maisha hadi sasa kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo.

Kaburi la umati lililotengwa katika jimbo la New York, Marekani kwa ajili ya wagonjwa wa Covid-19

"Watu wanakufa, hilo ni kweli" amekiri Trump katika mahojiano na tovuti ya habari ya Axios na kuongeza kuwa: "Ndivyo hali ilivyo. Lakini haimaanishi kwama hatufanyi kila tuwezalo. Unadhibitiwa kadiri unavyoweza kuudhibiti. Hili ni janga la kutisha."

Nchini Brazil Rais Jair Bolsonaro ameendelea kupinga uwekaji kafyu hata baada ya yeye mwenyewe na mawaziri kadhaa wa serikali yake kubainika kuwa na virusi vya corona.

Hata katika baadhi ya maeneo ya dunia ambako usambaaji wa virusi vya corona ulionekana kudhibitiwa, nchi za maeneo hayo, hivi sasa zinasajili visa kadhaa vipya vya watu walioambukizwa ndani ya siku moja, ikiwa ni ishara kuwa, mapambano dhidi ya virusi hivyo yatachukua muda mrefu.../

 

Maoni