Aug 06, 2020 11:16 UTC
  • Facebook yafuta video ya kupotosha ya Donald Trump kuhusu virusi vya corona

Mtandao wa kijamii wa Facebook umefuta video iliyorushwa hewani na Rais Donald Trump wa Marekani akidai kuwa watoto hawapatwi na virusi vya corona!

Taarifa iliyotolewa jana na Facebook ilisema kuwa, video hiyo inakiuka kanuni za shirika hilo kuhusu upashaji habari za kupotosha kuhusiana na virusi vya corona. Hatua hii ya Facebook inafuatia ile iliyochukuliwa na Twitter jana Jumatano ya kufunga kwa muda ukurasa rasmi wa kampeni za urais za Donald Trump baada ya kuandika habari ya kupotosha umma kwamba virusi vya corona haviwapati watoto.

Msemaji wa Facebook amesema kuwa video iliyowekwa na Donald Trump katika ukurasa wa mtandao huo wa kijamii ina madai ya uongo yanayosisitiza kuwa tabaka fulani la watu halipatwi na virusi vya corona, jambo ambalo ni ukiukaji wa sera za Facebook kuhusiana na taarifa za uongo kuhusu virusi vya corona.

Msemaji wa timu ya kampeni ya Trump, Courtney Parella, amedai kampuni ya Facebook inachukua msimamo dhidi ya kiongozi huyo wa Marekani.

Madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba watoto hawapatwi na virusi vya corona yanakwenda kinyume na uchunguzi wa kisayansi wa taasisi muhimu za kitaifa na kimataifa.

Uchunguzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliofanywa duniani kote kwa kutilia maanani wagonjwa milioni sita wa virusi vya corona umebaini kuwa, watoto wenye umri wa kati ya miaka 5 na 14 wanaunda asilimia 4.6 ya waathirika wote wa virusi hivyo.

Tags

Maoni