Aug 09, 2020 03:18 UTC
  • Hitilafu kali za Ujerumani na Ufaransa dhidi ya Marekani kuhusu marekebisho katika shirika la WHO

Kushindwa serikali ya Rais Donald Trump kudhibiti maambukizi ya virusi vya COVID-19 nchini Marekani kumemfanya rais huyo ajaribu kuwepa lawama za kufeli huko kwa kulituhumu Shirika la Afya Duniani WHO kuwa lilifeli katika utekelezaji wa majukumu yake.

Katika uwanja huo Trump karibuni hivi aliamua kulikatia shirika hilo msaada wa kifedha na hatimaye kujitoa katika shirika hilo muhimu la kimataifa huku akitaka marekebisho ya msingi yafanyike ndani ya shirika hilo, jambo ambalo limeibua hitilafu kubwa kati ya nchi hiyo na washitrika wake wa Ulaya.

Katika kulalamikia hatua hiyo, Ufaransa na Ujerumani hivi karibuni zilijitoa katika mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kuhusu marekebisho hayo ambapo Marekai ilitaka kuyaongoza. Nchi mbili hizo muhimu za Ulaya zililalamika vikali zikidai kwamba Marekani ilitaka kuongoza mchakato wa marekebisho hayo ilihali ilikuwa imejitoa yenyewe katika uanachama wa shirika hilo.

Bila shaka hatua hiyo ya nchi za Ulaya ni ishara nyingine ya wazi kuwa Trump kwa mara nyingine tena imefeli katika juhudi zake za kutaka kutumia mabavu na nguvu kusukuma mbele siasa zake za upande mmoja katika ngazi za kimataifa. Kwa sasa Marekani ndiyo mwenyekiti wa kundi la G7 na imekuwa na matumaini makubwa ya kutumia nafasi yake hiyo katika kuainisha mfumo wa utendaji wa WHO. Marekani inataka kuongoza mchakato wa marekebisho katika shirika hilo la afya katika hali ambayo imekuwa ikilituhumu kuwa lina ushirikiano wa karibu sana na China na kwamba limefeli katika majukumu yake ya kudhibiti ueneaji wa virusi vya corona duniani, tuhuma ambazo zmekanushwa na maafisa wa ngazi za juu wa shirika hilo.

WHO inatuhumiwa na Marekani kuwa na uhusiano wa karibu na China

Hata kama viongozi wa Ulaya wamelikosoa shirika hilo kwa maneno ambayo ni laini kidogo yakilinganishwa na ya Marekani, lakini wamekuwa wakikosoa hatua ya upande mmoja ya Trump dhidi ya shirika hilo na kusema kuwa huenda ikadhoofisha nafasi ya shirika hilo muhimu katika ngazi za kimataifa.

Ungaji mkono wa wazi wa Umoja wa Ulaya kwa Shirika la Afya Duniani mkabala na vitisho vya Trump ni jambo linalothibitisha wazi kwamba hata washirika muhimu wa Marekani barani Ulaya wamechoshwa na hatua zisizo za kisheria na za upande mmoja za serikali ya Washington dhidi ya taasisi na mashirika muhimu ya kimataifa. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba badala ya Trump kulisaidia shirika hilo ambalo lina nafasi muhimu katika kudhibiti magonjwa mbalimbali duniani yakiwemo ya kuambukiza na kusaidia kuratibu mipango ya serikali tofauti kwa ajili ya kukabiliana na maradhi hayo, amechukua uamuzi usio wa kimantiki wa kulikatia msaada wa kifedha na kisha kujivua uanachama wa shirika hilo. Hatua hiyo ya Trump imekosolewa vikali ndani na nje ya Marekani.

Nancy Pelosi, Spika wa Congress ya Marekani amesema: Hatua ya Trump kulikatia msaada wa fedha Shirika la Afya Duniani, ni hatari na ni jambo linalokiuka sheria. Ni wazi kuwa hatua hiyo inahatarisha maisha ya Wamarekani na ya watu wengine ulimwengini.

Hatua ya Trump kusimamisha misaada yake ya kifedha na kisha kujitoa katika Shirika la Afya Duniani WHO imekosolewa vikali na jamii ya kimataifa zikiwemo nchi za Ulaya. Nchi hizo zinaamini kwamba hatua hiyo ya Marekani inakwenda kinyume na misingi ya maadili na ahadi zake za kizisaidia taasisi muhimu za kimataifa na hasa katika mazingira ya hivi sasa ya kuenea virusi hatari vya corona katika karibu nchi zote za dunia. ‎Jens Spahn, Waziri wa Afya wa Ujerumani amekosoa uamuazi wa Marekani kujitoa katika shirika la WHO na kusema kuwa hatua hiyo ni ya kukatisha tamaa kwa mfumo wa afya duniani.

Jens Spahn

Nukta muhimu hapa ni kuwa washirika wote wa Marekani wameungana na kukosoa hatua yake hiyo dhidi ya WHO. Kabla ya hapo pia washindani muhimu wa Marekani yaani Russia na China zilipinga vikai hatua hiyo ya upande mmoja ya Marekani na kuzitaka nchi nyingine za dunia ziongeze misaada yao ya kifedha kwa shirika hilo muhimu linaloshughulikia masuala ya afya duniani. Ni wazi kuwa hatua ya karibuni ya Ujerumani na Ufaransa ya kujitoa kwenye mazungumzo ya kurekebisha mfumo wa utendaji wa WHO, kama alama ya kulalamikia siasa za Trump kuhusiana na shirika hilo, si tu kwamba imetoa pigo kubwa kwa nafasi ya Marekani na Trump bali ni ishara inayoonyesha wazi kwamba nguvu na ushawishi wa Washington kwa washirika wake wa Ulaya ili waweze kushirikiana nayo kuhusu masuala tofauti ya kimataifa, unaendelea kupungua siku baada ya nyingine.

Tags

Maoni