Aug 10, 2020 11:01 UTC
  • Safari ya waziri wa Marekani Taiwan; kuongezeka mvutano kati ya China na Marekani

Licha ya upinzani mkali wa China, Waziri wa Afya na Huduma za Kibinadamu wa Marekani jana Jumapili alifanya safari huko Taiwan akiwa ameandamana na ujumbe wa ngazi za juu wa nchi hiyo.

Hiyo ni safari ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani huko Taiwan katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Tangu mwaka 1979 hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa serikali ya Marekani aliyekuwa amewahi kufanya safari katika kisiwa hicho ambacho kinatambulika rasmi kimataifa kuwa chini ya mamlaka ya China. Marekani ilikata uhusiano wake wa kidiplomasia na kisiwa hicho mwaka 1979 na kuitambua rasmi serikali ya kikomunisti ya Beijing kuwa mwakilishi halisi wa China moja inayojumuisha kisiwa cha Taiwan. Pamoja na hayo, Waziri wa Afya wa Marekani amefanya safari katika kisiwa hicho bila ya ruhusa ya serikali ya Beijing kwa madai ya kuimarisha uhusiano na viongozi wa kisiwa hicho katika kukabiliana na janga la virusi vya corona.

Hata kama Taiwan sio mwanachama wa Shirika la Afya Duniani WHO kutokana na upinzani wa China, lakini imefanikiwa pakubwa katika kupambana na virusi vya corona. Kufikia sasa imeripoti visa 500 tu vya corona na kusajili vifo 7 vinavyotokana na maradhi hayo na karibu taasisi zake zote za kielimu na kimasomo, kiutamaduni, kiuchumi na vituo vya umma vinaendelea na shughuli zao za kawaida.

Alex Azar (kushoto) akizungumza na Rais Tsai Ing-wen wa Taiwan mjini Taipei, Jumatatu 10,2020

Hata kama Alex Azar, Waziri wa Afya wa Marekani amefanya safari huko Taiwan kwa kisingizio cha kuimarisha ushirikiano kuhusu corona lakini ni wazi kuwa safari hiyo imefanyika katika mazingira ambayo miezi ya hivi karibuni imeshuhudia mvutano mkubwa kati ya Washington na Beijing. Kuongezeka vita vya kibiashara kati ya China na Marekani na wakati huohuo tuhuma kali za Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya China kuwa ilificha habari muhimu kuhusu kuenea virusi vya corona ni baadhi ya sababu ambazo zimeibua mgogoro mkubwa katika uhusiano wa nchi mbili.

Taiwan, Tibet na Hong Kong ni mstari mwekundi wa China katika mahusiano yake na nchi za kigeni. China inaichukulia Taiwan kuwa 'mkoa wake ulioasi' hivyo hukabiliana vikali na juhudi zozote za kutaka kutambua rasmi kujitawala kwake. Mara kwa mara imekuwa ikipinga safari za maafisa wa Marekani na mauzo ya silaha ya nchi hiyo kwa kisiwa hicho na kulaani vikali uhusiano rasmi wa nchi za kigeni na kisiwa hicho. Ndio maana ikalaani vikali safari iliyofanywa sasa na Waziri wa Afya wa Marekani katika kisiwa hicho.

Katika uwanja huo, Wang Wenbin, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema: China inapinga vikali mawasiliano yoyote rasmi kati ya Marekani na Taiwan na tayari imewasilisha malalamiko yake kwa serikali ya Trump. Washington inapasa kujiepusha kuharibu uhusiano wa China na Marekani.

Safari ya Waziri wa Afya wa Marekani katika kisiwa cha Taiwan inaweza kuchukuliwa kuwa ni juhudi mpya zinazofanywa na Marekani kwa madhumuni ya kuibana na kuzidisha mashinikizo dhidi ya China. Trump ambaye umashuhuri wake umapengua sana nchini Marekani kutokana na kushindwa kukabiliana vilivyo na virusi vya corona na wala hana wakati wa kutosha wa kufanya kampeni kabla ya kufayika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ifikapo mwezi Novemba, ameamua kutekeleza siasa mpya za kuichokoza China ili aweze kuboresha nafasi ya kushinda uchaguzi huo.

Manowari za China zikifanya mazoezi ya kijeshi katika Lango Bahari la Taiwan

Kabla ya kufanyika safari ya Azar huko Taiwan, Trump aliishambulia vikali China kwa maneno na kudai bila kutoa ushihidi wowote wa kinyaraka kwamba huenda ulisambaza kwa makusudi virusi vya corona duniani. Alisema kwamba China ilidhibiti na kuzuia kuenea virusi hivyo katika ardhi yake lakini wakati huo huo ikavisambaza kwa makusudi katika maeneo mengine ya dunia.

Kwa kutumia mbinu hiyo chafu, Trump anataka kuzidisha mashinikizo dhidi ya China na kufunika kufeli kwake katika kudhibiti virusi cya corona nchini Marekani ili kwa njia hiyo aweze kujipa itibari mbele ya Wamarekani. Hivyo ni wazi kuwa moja ya malengo ya safari ya Waziri wa Afya na Huduma za Kibinadamu wa Marekani kisiwani Taiwan ni kuvutia uungaji mkono wa Wamarekani kwa Trump kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa rais nchini humo mwezi Novemba. Pamoja na hayo ni bayana kuwa kinyume na anavyotarajia Trump, Safari hiyo itaongeza tu mvutano uliopo baina ya nchi mbili na kuendelea kuharibu uhusiano wao.

Tags

Maoni