Aug 10, 2020 13:16 UTC
  • Juan carlos akiwa pamoja na mfalme wa zamani wa Saudia, Abdullah bin Abdul Aziz
    Juan carlos akiwa pamoja na mfalme wa zamani wa Saudia, Abdullah bin Abdul Aziz

Wananchi wa uhispania wamefanya maandamano wakitaka kukomeshwa utawala wa kifalme nchini humo baad aya mfalme wa zamani wa nchi hiyo, Juan Carlos kuondoka nchini humo ghafla akiandamwa na kashfa ya ufisadi unaohusisha utawala wa kifalme wa Saudi Arabia.

Maandamano hayo yamefanyika katika mji wa Valencia huku wakazi wa Mallorca wakipanga kuitisha maandamano kama hayo wiki hii wakati wa ziara ya Mfalme Felipe kisiwani humo.

Juan Carlos aliyeng'atuka na kumwachia kiti cha ufalme wa Uhispania mtoto wake, Felipe hapo mwaka 2014, Jumapili iliyopita alitangaza ghafla uamuzi wake wa kuondoka nchini humo na kuzusha maswali mengi kuhusu mustakbali wa utawala wa kifalme wa Uhispania. Ripoti zinasema kuwa mfalme huyo wa zamani wa Uhispania anaishi katika mojawapo ya hoteli ghali zaidi duniani katika mji mkuu wa Imarati, Abu Dhabi.

Gazeti la Times la Uingereza limeandika kuwa maisha Juan Carlos yaliyoanzia uhamishoni huwenda yakamalizikia uhamishoni.

Mfalme Felipe wa Uhispania akiwa pamoja na baba yake, Juan Carlos.

Mwezi Juni mwaka huu Mahakama Kuu ya Uhispania ilifungua uchunguzi kuhusu madai ya kuhusika Juan Carlos katika mkataba wa ujenzi wa reli ya kasi kubwa inayounganisha miji ya Makka na Madina nchini Saudi Arabia.

Gazeti la La Tribune de Genève la Uswisi lilifichua kuwa mfalme huyo wa zamani wa Uhispania alipokea mlungula wa dola milioni 100 kutoka kwa mfalme wa zamani wa Saudi Arabia.

Wafalme wa Uhispania wana kinga ya kufikishwa mahakamani wanapokuwa madarakani lakini Juan Carlos alijiengua na kukabidhi madaraka kwa mwanaye, Felipe mwaka 2016; hivyo anaweza kupandishwa kizimbani.

Maoni