Aug 12, 2020 02:31 UTC
  • Sisitizo la kuongezwa ushirikiano wa Iran na Venezuela na ghadhabu za Washington kwa hilo

Katika miaka ya hivi karibuni Iran na Venezuela zimeandamwa na vikwazo vya kiuchumi na kisiasa vya Marekani na viongozi wa White House wamefanya juhudi kubwa kutumia nyenzo mbalimbali ili wazifanye nchi mbili hizi zisalimu amri na kufuata siasa za Washington.

Hata hivyo siasa hizo za Washington dhidi ya Ira na Venezuela si tu kwamba, zimefeli na kugonga ukuta, bali mataifa hayo yamekuwa na uhusiano imara na wa kirafiki zaidi na sasa zimekuwa zikichukua hatua katika njia ya kukabiliana na vikwazo na mashinikizo ya Marekani.

Katika uwanja huo, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ametoa taarifa kwa mnasaba wa miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia wa Iran na nchi yake na kutangaza kuwa, katika kipindi cha miaka yote hii uhusiano wa pande mbili umeimarika zaidi na kumeundika udugu usiotetereka baina ya mataifa haya mawili huku suala la kutetea mamlaka ya kujitawala likiimarika.

Mataifa ya Amerika ya Latini hususan zile nchi ambazo zinaongozwa na serikali ya mrengo wa kushoto zinazopigania uadilifu na zilizo dhidi ya ukoloni, kwa muda mrefu sasa zimekuwa zikizingatiwa na Marekani. Viongozi wa Washington wanafanya juhudi za kutumia mbinu mbalimbali kama vile kuunga mkono mapinduzi, uharibifu wa kimitandao, kutoa himaya kwa makundi ya upinzani ndani ya mataifa hayo, kutumia vitisho vya kijeshi sambamba na kutekeleza vikwazo vikali dhidi ya serikali hizo ili kuzifanya ziitii Marekani au kuingiza madarakanai serikali ambazo zitakuwa vibaraka wa White House kama kile kilichotokea katika miaka ya hivi karibuni huko nchini Bolivia.

Bendera bza Iran na Venezuela

Ukweli wa mambo ni kuwa mataifa ya Amerika ya Latini yana umuhimu mkubwa mno kwa Maekani katika upande wa kulinda na nafasi ya Washington na hivyo kustafidi na vyanzo vya utajiri wa mataifa hayo. Nchi ya Venezuela katika kipindi cha hususan mwaka mmoja uliopita, imeandamwa na mashinikizo maradufu ya Marekani. Vikwazo vya kifedha, kibenki, vikwazo katika sekta ya nishati, Marekani kuwasaidia wapinzani kutangaza kuwa pamoja nao, kumtambua rasmi Juan Guaido kiongozi wa upinzani wa Venezuela kuwa Rais wa nchi na kutoa himaya ya kila upande kwa mpinzai huyo, kulipelekea matatizo ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo yashadidi zaidi.

Katika miezi ya hivi karibuni sambamba na kuenea virusi vya corona ulimwenguni na kutawala mazingira maalumu ya kiuchumi na kiutabibu, Marekani imeendelea kuishinikiza Venezuela na kupuuza maelekezo yaliyotolewa na mashirika mbalimbali ya kimataifa ya kuondoa mashinikizo hayo hasa katika kipindi hiki na kutanguliza mbele ubinadamu.

Ukweli wa mambo ni kuwa, viongozi wa Marekani ambao hadi sasa wameshindwa kuipundua serikali ya mrengo wa kushoto ya Nicolas Maduro, wangali wanajitutumua na kutumia fimbo ya kiuchumi na mashinikizo ili kupunguza himaya na uungaji mkono wa wananchi kwa kiongozi huyo na hivyo kupiga hatua kuelekea katika malengo yao.

Meli ya mafuta ya Iran ikielekea Venezuela

Katika mazingira kama haya, ushirikiano wa Iran na Venezuela umechukua wigo mpana zaidi. Iran daima imekuwa mtetetezi wa wapigania uhuru na chuki dhidi ya ukoloni duniani na kwa miaka mingi imekuwa na uhusiano wa karibu na nchi hiyo ya Amerika ya Latini. Hivi sasa na baada ya kushadidi matatizo ya kiuchumi nchini Venezuela likiwemo suala la uhaba wa nishati ya mafuta, licha ya vitisho vya Marekani, Iran imepeleka katika bandari ya Venezuela meli tano za mafuta. Kuwasili kwa meli hizo za mafuta nchini Venezuela, kulitatua sehemu muhimu ya uhaba wa fueli nchini humo, jambo ambalo limewakasirisha mno viongozi wa Marekani.

Jorge Arreaza, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela amesisitizia mshikamano na mfungano wa Tehran na Caracas katika anga ya vikwazo na mashinikizo haramu, chuki na hatua za upande mmoja ya Marekani dhidi ya Venezuela na kusema kuwa: Muamala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ujumbe wa heshima na izza kwa ulimwengu, ujumbe ambao unaweza kuwa kiigizo cha watu ambao wanaendesha mapambano dhidi ya ubeberu.

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela

Iran na Venezuela kwa kupanua ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi zikitumia uwezo wao zinalenga kuyapatia ufumbuzi matatizo zinayokabiliwa nazo na kuvuka vizingiti vinavyosababishwa na siasa za chuki za Marekani. Uhusiano wa Iran na Venezuela unaimarishwa katika hali ambayo, viongozi wa Washington wangali wanaendeleza siasa za kukabiliana na mataifa haya mawili.

Kuteuliwa hivi karibuni Elliott Abrams ambaye ni mjumbe wa Marekani katika masuala ya Venezuela kuwa mwakilishi maalumu wa Washington katika masuala ya Iran ni hatua ambayo kwa upande mmoja inaonyesha lengo la Washington la kuedeleza mashinikizo dhidi ya mataifa haya mawili na kwa upande wa pili inaweka wazi kuchanganyikiwa na kukosa muelekeo sera za kigeni za Rais Donald Trump mkabala wa Tehran na Caracas. Inaonekana kuwa, kuongezeka ushirikano wa Iran na Venezuela kumezidi kuwakasirisha viongozi wa Marekani.

Tags

Maoni