Aug 12, 2020 08:08 UTC
  • Kuarifishwa Harris  kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa  Marekani

Kama ilivyokuwa imetabiriwa, Joe Biden mgombea mkuu wa chama cha Democrat katika uchaguzi wa Rais wa Marekani mwaka huu wa 2020 amemuarifisha Seneta Kamala Harris kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais nchini humo.

Kufuatia uamuzi huo, Joe Biden na Kamala Harris watachuana katika uchaguzi wa Novemba Tatu mwaka huu na Donald Trump na Mike Pence wagombea wa chama cha Republican.  

Donald Trump na Mike Pence, Wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais kwa tiketi ya chama cha Republican

Harris ni mwanamke wa tatu katika historia ya Marekani anayejaribu karata yake ya kuwania kiti cha Makamu wa Rais nchini Marekani. Wakati huo huo ni mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika na wa kwanza mwenye asili ya Asia kuarifishwa na moja ya vyama viwili vikubwa nchini Marekani kushiriki katika uchaguzi wa Rais nchini humo. Bi Harris ana asili ya Kiafrika kupitia baba yake ambaye ni Mjamaica na mama yake ni Mhindi ambaye anatokea barani Asia. Kwa kuzingatia asili hiyo ya mchanganyiko wa kifamilia, hatua ya Biden ya kumuarifisha Kamala Harris inaimarisha nafasi ya wagombea wa chama cha Democrat miongoni mwa wanawake wenye asili ya Kiafrika, Asia na makundi mengine mengi na ya kikabila huko Marekani. Aidha  Harris Kamala  anahesabiwa kuwa shakhsiya wa umri wa wastani kwa kuwa na  miaka 55 ukilinganisha na umri wa Joe Biden aliye na miaka 77. Kipimo cha umri cha makamu huyo wa Biden kina umuhimu kutokana na kuwa, iwapo Biden atafanikiwa kuingia White House atakuwa miongoni mwa Marais wenye umri mkubwa zaidi wa Marekani; na huenda akashindwa kushiriki kwa muhula wa pili katika uchaguzi wa Rais wa mwaka 2024 wakati huo ambapo atakuwa na miaka 82. Kwa msingi huo Harris akiwa Makamu wa Rais, ana nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2024.  

Hata hivyo timu ya Biden na Harris ingali inakabiliwa na njia ngumu ili kuishinda timu ya Trump na Pence na hivyo kuingia White House. Pamoja na kuwepo migogoro na matatizo mbalimbali makubwa yaliyosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona; ukosefu mkubwa wa ajira na ghasia kubwa kuhusu vitendo vya ubaguzi wa rangi huko Marekani hakuna uhakika iwapo Wademocrat wataweza kuibuka washindi dhidi ya Warepublican.  Aidha ni vigumu kuthibitisha iwapo Wademocrat wataibuka na ushindi kutokana na shakhia ya upole ya Biden, kampeni za kusuasua za chama hicho na baadhi ya udhaifu katika utendaji wa Kamala Harris licha ya Wademocrat kuongoza katika chunguzi za maoni.  

Joe Biden na Harris Kamala, wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wake kwa tiketi ya chama cha Democrat 

Aidha inatazamiwa kuwa katika siku zijazo Wahafidhina wataanzisha mashambulio makali  dhidi ya Harris Kamala. Pamoja na hilo, Trump ameonekana kuanzisha mashambulizi dhidi ya mwanamama huyo muda mfupi baada ya kuarifishwa kuwa mgombea mwenza wa Biden. Trump  amemtaja Bi Harris kuwa mtu dhaifu anayefikiria kuongeza kodi, kupunguza bajeti ya ulinzi na kuvisambaratisha vikosi vya polisi; masuala ambayo yana umuhimu kwa Wahafidhina wa Marekani. Aidha inatazamiwa kuwa, utendaji wa Harris katika nafasi za kisheria katika jimbo la Calfornia unatarajiwa kumulikwa na mahasimu wa chama cha Republican hasa kwa kutilia maanani kuwa baadhi ya hukumu alizowahi kutoa zilikuwa dhidi ya raia weusi na wale wa jamii ya Kilatini. 

Ala Kul haal, zimesalia karibu siku 80 hadi kufanyika uchaguzi wa rais nchini Marekani. Katika muda huo, wagombea wa kiti cha urais wa vyama vyote watakuwa na mdahalo mara tatu kwa njia ya televisheni; na wagombea wa nafasi ya Makamu wa Rais watakuwa na mdahalo mara moja. Ndio maana mdahalo wa televisheni kati ya Harris na Pence uliopangwa kufanyika Oktoba 10 mwaka huu ukatajwa kuwa na umuhimu mkubwa katika kuvutia maoni ya wapiga kura wa Marekani. 

 

Maoni