Aug 13, 2020 06:39 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani yuko katika duru nyingine ya safari barani Ulaya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ameanza duru mpya ya safari barani Ulaya baada ya safari nyingine wiki tatu zilizopita. Mara hii Pompeo anatembelea nchi nne za Ulaya ya Kati na Mashariki.

Pompeo ameanza safari yake hiyo kwa kuitembelea Jamhuri ya Czech ambapo aliwasili mjini Prague Jumanne kwa safari ya siku mbili. Baada ya hapo atazitembelea Slovenia, Austria na Poland. Maudhui muhimu za safari ya Pompeo zimetajwa kuwa ni kupeleka wanajeshi zaidi wa Marekani nchini Poland, mfumo wa kisasa wa simu za mkononi wa 5G na kutotegemea nishati ya Russia. Malengo ya kistratijia katika safari ya Pompeo na wakuu wengine wa Marekani katika mazungumzo na nchi za Ulaya ni kueneza chuki dhidi ya China na Russia.

Katika safari yake ya wiki tatu zilizopita barani Ulaya, Pompeo alikutana na wakuu wa Uingereza na Denmark ambapo alitaka nchi hizo mbili zisishirikiane na shirika la mawasiliano la Huawei la China hasa katika uga wa kusambaza mfumo wa intaneti ya simu za mkononi wa kizazi cha tano yaani 5G.

Bomba la gesi la Nord Stream

Akiwa Denmark pia Pompeo aliitaka nchi hiyo isishiriki katika mradi wa ujenzi wa bomba la gesi la Nord Stream 2 ambalo linapitisha gesi yake Denmark kuelekea katika maeneo mengine ya Ulaya. Mabomba ya  gesi ya Nord Stream 2 na Nord Stream 1 yatatumika kufikisha gesi ya Russia nchini Ujerumani na nchi zingine za Ulaya. Umuhimu wa  bomba la Nord Stream ni kuwa litapunguza utegemezji wa Ujerumani na nchi zingine za Ulaya kwa gesi ya Russia ambayo inapitia Ukraine nchi ambayo hukumbwa na misukosuko mingi ya kisiasa. Bomba la Nord Stream linaenda kinyume na sera za kistratijia za Marekani za kuibua misiguano na ufa baina ya Russia na Ulaya.

Marekani daima imekuwa ikiitizama Russia kama adui wake na inahitajia Ulaya ili kutekeleza sera hiyo ya uhasama.

Marekani inatekeleza sera ya kuimarisha satwa ya muungano wa kijeshi wa NATO katika eneo la mashariki mwa Ulaya ili kufikia malengo yake ya kuizingira mipaka ya Russia.

Hivi sasa ni wazi kuwa Marekani haiwezi kuzitegemea tena Ufaransa, Uingereza na Ujerumani na hivyo inatafuta washirika wapya wenye kutegemewa. Ikumbukwe kuwa baada ya Ujerumani na Ufaransa kukataa kushirikiana na Marekani katika uvamizi wa Iraq, Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld alisema zama za kile alichokitaja kuwa 'Ulaya ya Kale' zilikuwa zimefika ukingoni huku akiashiria kuhusu kuibuka 'Ulaya Mpya'. Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alibadilisha wigo wa usalama wa Marekani kutoka magharibi hadi mashariki mwa Ulaya ambapo aliwasilisha mpango wa ngao ya makombora kwa ajili ya Poland na Jamhuri ya Check. Mpango huo ulikabiliwa na upinzani na vitisho kutoka Russia huku Ujerumani na Ufaransa zikikataa kushirikiana na Marekani katika utekelezwaji wake. Donald Trump sasa anafuatilia kwa uzito suala la kuwapa nguvu waitifaki wapya barani Ulaya kwa kutumia msingi wa chuki dhidi ya Russia na China. Hivi sasa Trump anazungumza kuhusu kutekeleza mpango kupunguza wanajeshi wa Marekani nchini Ujerumani na kuwahamishia Poland. Katika safari ya Pompeo nchini Poland, mapatano kuhusu kutumwa wanajeshi wa Marekani yanatazamiwa kutiwa saini. Hata kama mgombea wa chama cha Democrats, Joe Biden, atashinda katika uchaguzi wa rais, hakutakuwa na mabadiliko katika sera hiyo mpya ya Marekani kuhusu Russia na Ulaya.

Baada ya Trump kutangaza kupunguza askari wa Marekani nchini Ujerumani, Heiko  Maas Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema: “Taharuki za sasa baina ya Ujerumani na Marekani hazitatatuliwa kwa kushindwa Trump katika uchaguzi ujao wa rais.”

Hali kadhalika chuki dhidi ya China ni sera nyingine inayofuatiliwa na Marekani barani Ulaya. Baada ya China kufanikiwa kuteka sehemu kubwa ya soko la Ulaya ilikuwa inakusudia kueneza mfumo wa intaneti ya simu za mkononi ya kizazi cha tano yaani 5G barani Ulaya. Marekani inapinga vikali mashirika ya China kueneza teknolojia hii muhimu barani Ulaya. Kwa msingi huo Marekani sasa inalenga kuvuruga uhusiano wa China na nchi za Ulaya.

Pamoja na hayo, viongozi wa nchi mbali mbali za dunia, hasa waitifaki wa Marekani barani Ulaya kama vile Ujerumani na Ufaransa, wanapinga wazi wazi matakwa ya Marekani na hiyo bila shaka ni ishara ya kuendelea kuporomoka nguvu za Marekani.

 

Tags

Maoni