Aug 13, 2020 13:56 UTC
  • Kitabu cha

Mwandishi mashuhuri wa habari wa Kimarekani Bob Woodward atazitoa hadharani barua 25 za binafsi ambazo rais wa nchi hiyo Donald Trump ameandikiana na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.

Tovuti ya habari za kisiasa ya TheHill imeripoti kuwa, Bob Woodward, mwandishi wa habari aliyefichua kashfa ya Watergate ataziweka hadharani barua 25 za binafsi alizoandikiana Rais Donald Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, ambazo hazijawahi hapo kabla kuripotiwa na vyombo vya habari. Woodward anatazamiwa kuzichapisha barua hizo katika kitabu chake cha pili kiitwacho "Ghadhabu" (Rage), baada ya kitabu chake cha kwanza alichoandika kuhusu Trump alichokipa jina la "Hofu" (Fear).

Kitabu hicho cha 'Ghadhabu' kinaonyesha kuwa, katika vipindi nyeti na hasasi vya uchukuaji maamuzi, majibu na hatua ambazo Trump amechukua katika migogoro na majanga yaliyotokea mwaka huu wa 2020 zimesukumwa na utashi wake, mazoea na tajiriba ya utendaji aliyopata katika kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo ya urais wake.

Trump alipokutana na Kim

Kitabu cha "Ghadhabu" cha Bob Woodward kinatazamiwa kutolewa tarehe 15 Septemba, zitapokuwa zimesalia wiki saba tu kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais wa Marekani.

Mwandishi huyo wa habari, ambaye ni mjumbe wa bodi ya wahariri ya gazeti la Washington Post alipata umaarufu baada ya kufichua ripoti ya kashfa ya Watergate.

Kashfa hiyo ya Watergate ilitokea Washington baina ya mwaka 1972 hadi 1975, ambapo baada ya kupamba moto na kuibua uwezekano wa kusailiwa, ilimlazimisha rais wa wakati huo wa Marekani Richard Nixon kujiuzulu wadhifa wake.../ 

Tags