Aug 14, 2020 02:51 UTC
  • Juhudi za Pempeo kuiarifisha China kama tishio kwa nchi za Ulaya

Tokea aingie madarakani mwezi Januari 2017, Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akitekeleza siasa kali na za uhasama dhidi ya China ambapo amekuwa akiendesha vita vya kisiasa, kibiashara na kiusalama dhidi ya nchi hiyo muhimu ya Asia.

Viongozi wa ngazi za juu wa serikali yake pia wamekuwa wakidumisha siasa hizo hizo ambapo wanafanya juhudi kubwa za kuidhihirisha China kuwa hatari kubwa kwa nchi za Magharibi.

Katika uwanja huo, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akizungumza katika bunge la Seneti la Jamhuri ya Czech hapo siku ya Jumatano alidai kwamba hatari ya China kwa nchi za Ulaya kwa sasa ni kubwa kuliko ya Muungano wa Sovieti katika kipindi cha Vita Baridi. Amesema: Kile kinachoendelea sio Vita Baridi vya Pili. Changamoto ya kusimama dhidi ya Chama cha Kikomonisti cha China ni kubwa zaidi. Ameendelea kusema: 'Chama cha Kikomonisti kina njia nyingi na kimekita mizizi katika uchumi wetu, siasa zetu na jamii zetu jambo ambalo halikuwepo wakati wa Muungano wa Sovieti.'

Pompeo anaashiria juhudi kubwa ambazo zimekuwa zikifanywa na China katika miaka ya karibuni kwa lengo la kuimarisha uhusiano, uwekezaji na ushirikiano na nchi za Ulaya, jambo ambalo si tu kuwa limepokelewa vizuri na Umoja wa Ulaya bali sasa Beijing inatekeleza mikakati kabambe ya kuwa na uhusiano mwema na kutekeleza miradi mingi muhimu ya maendeleo na nchi za Ulaya na hasa za mashariki mwa bara hilo kwa maslahi ya pande mbili. Safari za mara kwa mara na vikao tofauti vinavyofanywa na viongozi wa ngazi za juu wa China na Ulaya vina madhumuni ya kufikia lengo hilo. Miongoni mwa miradi maalumu inayofuatiliwa na China katika nchi za Ulaya ni kuanzisha katika nchi hizo mfumo wa mawasiliano ya simu ya kizazi cha tano yaani G5.

Shirika la mawasiliano ya simu la China, Huawei

Suala hilo ni kengele ya hatari kwa Marekani ambayo sasa imeanzisha hararakati kubwa za kutoa mashinikizo dhidi ya viongozi wa nchi hizo ili wasiruhusu kuenea ushawishi wa kiuchumi na kibiashara wa China katika nchi hizo. Marekani inazitisha nchi hizo kuwa zitakabiliwa na jibu kali la Washington la ima kupunguza uhusiano au hata kuziwekea vikwazo iwapo hazitatii amri ya Marekani ya kupunguza ushawishi wa China barani Ulaya.

Kwa hakika moja ya malengo ya safari ya Pompeo barani Ulaya ni kuzionya nchi za bara hilo zisiimarishe uhusiano wao na China. Pamoja na vitisho hivyo vya Marekani dhidi ya nchi za Ulaya lakini ni wazi kuwa nchi nyingi za bara hilo, ispokuwa Uingereza ambayo ina maslahi maalumu na Marekani, hazikubaliani kabisa na matakwa hayo ya Marekani na zinaona kuwa maslahi yao yako katika kudumisha ushirikiano na China. Charles Michel, Mkuu wa Baraza la Ulaya anasema: Uhusiano wa Umoja wa Ulaya na China umepiga hatua kubwa katika miaka ya hivi karibuni na utegemezi wetu wa kiuchumi ni mkubwa. Tunapaswa kushirikiana sote katika kukabiliana na changamoto muhimu za kimataifa kama vile mabadiliko ya tabianchi, kufikiwa ustawi endelevu na kupambana na virusi vya corona.

Charles Michel, Mkuu wa Baraza la Ulaya

Wakati huohuo kwa kuzingatia kupanuka kila siku pengo lililopo kati ya nchi za pande mbili za Bahari ya Atlantic, hivi sasa Umoja wa Ulaya unatafuta mshirika mwingine mbadala wa kibiashara na kiuchumi atakayechukua nafasi ya Marekani, ambaye kwa sasa si mwingine bali ni China ambayo ina uwezo mkubwa wa kiuchumi na uwekezaji. Kwa hakika mwenendo wa kuimarishwa uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Ulaya na China umeimarika sana katika miaka ya karibuni jambo ambalo limeikera sana Marekani na kuifanya ianzishe vita vya kibiashara na kisaikolojia dhidi ya China.

Uzeofu unaonyesha kwamba serikali ya Rais Trump wa Marekani ambayo huwa haizingatii sheria zozote za kimataifa, itazishinikiza nchi za Ulaya hadi zikubaliene na matakwa yake, la sivyo, itaamua kutumia mbinu zingine za mabavu kama vile vikwazo na kupunguza uhusiano na nchi hizo. Kama anavyosema Alexander Vintikov, Naibu Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa La Russia; Marekani haitasita kuzinyamazisha nchi za Ulaya katika kufuatilia malengo na maslahi yake.

Tags

Maoni