Aug 14, 2020 08:06 UTC
  • Iran yakanusha madai kuwa Marekani imeteka meli zake za mafuta

Balozi wa Iran mjini Caracas amekanusha madai ya gazeti la The Wall Street Journal kuwa, Marekani imeziteka meli nne zenye mafuta ya Iran ambazo zilikuwa zikielekea Venezuela.

Katika taarifa kupitia ukurasa wake wa Twitter, Balozi Hojjat Soltani amekanusha ripoti hizo za kutekwa meli zenye mafuta ya Iran ambazo zilikuwa zinaelekea Venezuela na kusema: "Huu ni uongo mwingine na vita vya kisaikolojia vya vyombo vya habari vya kipropangda vya utawala wa kibeberu wa Marekani." Soltani amesema meli hizo zinazodaiwa kutekwa si za Iran na pia wamiliki wao hawana uhusiano wowote na Iran na wala hazina bendera zinazohusiana na Iran.

Soltani ameongeza kuwa, rais gaidi wa Marekani asieneze habari na taarifa bandia ili kufidia kushindwa na kudhalilishwa na taifa kubwa la Iran.

Gazeti la Wall Street Journal lilichapisha taarifa Alhamisi na kusema utawala wa Trump kwa mara ya kwanza umechukua udhibiti wa meli ambazo zilikuwa na mafuata ya Iran kinyume cha vikwazo.  

Moja ya meli iliyofikisha mafuta ya Iran nchini Venezuela hivi karibuni pamoja na kuwepo vitisho vya Marekani.

Hivi karibuni na katika hatua ya kuisaidia na kuiunga mkono serikali na wananchi wa Venezuela waliowekewa mzingiro wa kiuchumi na Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilituma nchini humo meli tano za mafuta zilizokuwa zimebeba shehena yenye jumla ya mapipa milioni moja na nusu ya mafuta.

Iran ilituma meli tano hizo za mafuta nchini Venezuela ili kumaliza uhaba wa mafuta katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini licha ya vitisho kadhaa vilivyotolewa na Marekani.

Maoni