Aug 14, 2020 09:52 UTC
  • Rashida Tlaib: Waislamu hawatahadaiwa na mapatano ya Trump na Netanyahu

Mbunge Mwislamu wa Kongresi ya Marekani, Rashida Tlaib, amepinga vikali hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa: Waislamu hawatahadaiwa na mapatano ya Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Rashida Tlaib amesema kuwa, mapatano ya Trump na Netanyahu hayapunguzi mashaka na maumivu ya Palestina bali yanayazidisha.

Rashida Tlaib ameandika hayo katika mtandao wa Twitter baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza habari ya kufikiwa mapatano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kuhusu kuanzishwa uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia baina ya pande mbili. Hatua hiyo imelaaniwa na harakati zote za mapambano ya ukombozi wa Palestina. 

Msemaji wa harakati ya Hamas, Naye Fauzi Barhum ametoa taarifa kuhusu njama inayotekelezwa na Marekani iliyopelekea kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Imarati na utawala wa Kizayuni na Israel na kusema: "Mapatano hatari baina ya UAE na Israel ni zawadi ambayo Abu Dhabi imepewa na utawala huo ghasibu wa Kizayuni kutokana na kuwasaliti Wapalestina."

Trump na Netanyahu

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa mapema leo Ijumaa na kusema: "Watu wanaodhulumiwa wa Palestina na mataifa yote yanayopenda uhuru duniani kamwe hayatasamehe kitendo cha kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu na utendao jinai wa Israel." Taarifa hiyo imesema kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel ni kuwa mshirika katika jinai za utawala huo.

Tags

Maoni