Aug 28, 2020 06:29 UTC
  • Safari ya Mike Pompeo kusini mwa Ghuba ya Uajemi na kukaririwa madai yasiyo na msingi wowote

Marekani daima ikiwa na lengo la kuendeleza uwepo wake wa kijiopolitiki katika eneo la Ghuba ya Uajemi imekuwa ikitumia vizingizio visivyokuwa na maana hususan kupiga kwake ngoma ya kueneza chuki chidi ya Iran.

Lengo la Washington ni kuzifanya nchi za kusini mwa Ghuba ya Uajemi ziwe tegemezi kwake kadiri inavyowezekana, na kwa muktadha huo kuandaa uwanja na mazingira ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya nchi hizo na utawala haramu wa Israel. Katika fremu hiyo, Mike Popmeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani akiwa katika mwenendelezo wa safari yake ya kiduru, juzi Jumatano aliwasili katika Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Mkataba wa amani baina ya Imarati na Israel unahesabiwa kuwa hatua moja kubwa kuelekea amani ya Asia Magharibi katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Baadhi ya weledi wa mambo wanasema kuwa, safari ya Mike Pompeo nchini Imarati imelenga kuweka uratibu kuhusiana na mipango kadhaa pamoja na kuandaa safari za hapo baadaye ambapo moja ya safari hizo ambayo inaratajiwa kufanyika hivi karibuni ni ya Benjamin Netanyahu Wzairi Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Safari hiyo inatarajiwa kufanyika sambamba na kufunguliwa rasmi ubalozi wa Israel huko Abu Dhabi.

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani alipokutana na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel

Jumatatu iliyopita Mike Pompeo akianza safari yake hiyo ya kiduru alielekea huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa utawala huo ghasibu akiwemo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Baada ya kutoka Israel, Pompeo alivuka bara la Asia na kuelekea Sudan huko barani Afrika kwa minajili ya kwenda kuwakinaisha viongozi wa serikali ya muda ya nchi hiyo ili waanzishe uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel. Aidha Jumanne iliyopita akiendelea na safari yake hiyo ya kiduru, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani aliwasili Manama mji mkuu wa Bahrain ambapo katika mazungumzo yake na mrithi wa kiti cha Ufalme wa nchi hiyo alibadilishana naye mawazo kuhusiana na matukio ya kieneo hususan suala la kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia na utawala vamizi wa Israel.

Wakati anawasili Manama, Pompeo aliitaja Iran kuwa ni tishio na akasisitiza ulazima wa kuweko umoja baina ya nchi za Ghuba ya Uajemi dhidi ya Tehran. Katika hatua iliyofuata, Pompeo akiwa nchini Imarati alitoa madai yasiyo na msingi wowote kuhusiana na eti matokeo mazuri ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Imarati na Israel.

Katika hali ambayo, Pompeo alidai kuwa, mkataba wa amani wa Imarati na Israel ni hatua kubwa zaidi kuelekea amani, ukweli wa mambo ni kuwa, viongozi wa nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Ghuba ya Uajemi  hususan watawala wa Abu Dhabi wamechukua hatua ambayo ni kinyume kabisa na misimamo ya wazi na thabiti ya Wapalestina ambao wanaendelea kutaabika na kuteseka kutokana na dhulma inayoongeza kila uchao inayofanywa dhidi yao na utawala ghasibu wa Israel. Viongozi wa Imarati wanaota ndoto za alinacha kwa kudhani kwamba, hatua hiyo ya khiana na usaliti ni ya manufaa na maslahi ya nchi yao.

Mazungumzo ya Mike Pompeo na Abdalla Hamdok Waziri Mkuu wa Sudan

Swali la msingi ni kuwa, kuna mafungamano gani baina ya uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia baina ya Imarati na Israel na suala la kupatikana amani katika eneo la Asia Magharibi? Tena katika mazingira ambayo, kila siku iendayo kwa Mungu utawala bandia wa Israel umekuwa ukipanua wigo wa hatua zake ghasibu dhidi ya ardhi za Wapalestina na hivyo kushadidisha mashinikizo ya kuwafukuza Wapalestina kutoka katika ardhi za mababu zao?

Kwa muktadha huo, haifahamiki hasa, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ametumia mantiki na kigezo gani kutoa madai ya kulifunganisha suala la kuanzishwa uhusiano wa kawaida wa Israel na Imarati na taathira chanya za jambo hilo katika kupatiwa ufumbuzi kadhia ya Palestina.

Muhammad Ayesh, mweledi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Kiarabu anasema: Serika ya Trump kupitia mkwe wake Jared Kushner ambaye ni mshauri wake pia imeanzisha mashinikizo dhidi ya nchi za Kiarabu ili zianzishe uhusiano rasmi na Israel na kwa msingi huo iandae mazingira ya kuboresha hali mbaya ya maisha inayowakabili Wazayuni hususan mgogoro wa kiuchumi unaoikabili dunia kufuatia janga la virusi vya Corona.

Wakati huo huo, tayari Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameshafanya mambo kinyume na ahadi yake kwa viongozi wa Imarati ambapo sambambana na kukana juu ya kuweko makubaliano yoyote yale ya kuakhirishwa mpango wa Tel-Aviv wa kumega ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuiunganisha na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu makubaliano ambayo yamekuwa yakidaiwa na viongozi wa Imrati, amesisitiza kupinga kuuziwa na Marekani utawala wa Abu Dhabi ndege ya kivita aina ya F-35.

Makubaliano ya Imarati na Israel ya kuanzisha uhusiano baina yao yameendelea kulaaniwa kila kona ya Ulimwengu wa Kiislamu

Wakati huo huo hatupaswi kusahau kwamba, Pompeo akiwa mmoja wa shakhsia muhimu katika timu ya White House katika mwaka wa uchaguzi ambapo Trump anahitajia mno kuonyesha mafanikio ya ndani na nje mbele ya wapiga kura ili awakinaishe wamchague tena, amefanya safari hiyo ya kieneo kwa ajili ya malengo hayo ya uchaguzi.

Katika safari yake hiyo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amezishajiisha nchi hizo za Kiarabu zifuate mkondo wa Imarati katika kuanzisha uhusiano na Israel ili kwa utaratibu huo White House iweze kutembea kifua mbele na kudai kwamba, imepata mafanikio makubwa katika uga wa siasa za kigeni kwa maslahi ya Israel. Hassan Hanizadeh, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi anasema: Mike Popmeo amefanya safari ya kieneo kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya Trump katika uchaguzi ujao wa Marekani. Trump na timu yake wanafanya kila wawezelo ili waweze kupata himaya na uungaji mkono wa lobi za Wazayuni na kwa msingi huo wajiandalie mazingira ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Rais Novemba mwaka huu.

Tags