Sep 04, 2020 07:22 UTC
  • Alexey Navalny
    Alexey Navalny

Umoja wa Ulaya na Marekani zimekuwa zikiishinikiza Russia kupitia njia ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa kuwaunga mkono wapinzani wa serikali ya Moscow na kutumia madai ya kutetea haki za binadamu.

Sasa madai kwamba serikali ya Russia imempa sumu kinara wa kambi ya upinzani, Alexey Navalny, ndiyo silaha mpya inayotumiwa katika vita vya vyombo vya habari na propaganda za nchi za Magharibi dhidi ya serikali ya Moscow.

Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin), Dmitry Peskov amekanusha vikali wazo lolote la kutaka kuibebesha Moscow dhima ya tukio hilo la kupewa sumu mwanasiasa huyo wa upinzani na kusema: Madai ya Ujerumani kuwa serikali ya Moscow ilihusika na jinai hiyo hayana msingi wowote. Peskov amesema: Kabla ya kupelekwa Berlin, Alexey Navalny hakupatikana na sumu ya aina yoyote katika mwili wake. Hata hivyo amesisitiza kuwa, Russia iko tayari kushirikiana na Ujerumani kwa ajili ya kuweka wazi ukweli kuhusu hali ya Navalny.

Alexey Navalny alipatwa na matatizo ya kiafya tarehe 20 mwezi uliopita wa Agosti akiwa kwenye ndege iliyokuwa ikielekea Moscow kutoka mji wa Tomsk huko Siberia na akalazwa hospitalini. Baadaye alipelekwa Ujerumani kwa ombi la serikali ya nchi hiyo.

Taarifa rasmi iliyotolewa na serikali ya Ujerumani imesema kuwa Alexey Navalny alipewa sumu hatari ya Novichok kwa nia ya kumuua na imeitaka Russia itoe maelezo kuhusu kadhia hiyo. 

Navalny

Mpinzani wa serikali ya Russia, Alexey Navalny daima amekuwa akiungwa mkono na Umoja wa Ulaya na Marekani na ana nafasi kubwa katika maandamano yanayofanyika katika miaka ya karibuni dhidi ya serikali ya Russia. Katika miaka ya karibuni nchi za Magharibi zimekuwa zikiituhumu Russia kuwa inaingilia masuala mengi ya kisiasa hususan chaguzi zinazofanyika katika nchi hizo, na Washington imeiwekea Moscow vikwazo kwa kisingizio hicho. Mtaalamu wa masuala ya siasa wa Russia Pavel Sharikov anasema: Miongoni mwa sababu za kuharibika uhusiano wa pande mbili wa Washington na Moscow ni kwamba Russia imekuwa maudhui ya ushindani wa kisiasa wa ndani ya Marekani. Hii ni licha ya kwamba nchi za Magharibi zenyewe zimekuwa zikiingilia masuala ya ndani ya Russia na kuwachochea wananchi wa nchi hiyo kufanya maandamano na ghasia hususan baada ya chaguzi mbalimbali. Balozi za nchi za Ulaya na Marekani zimekuwa na nafasi muhimu katika kuchochea ghasia na machafuko hayo.     

Uchochezi huo wa nchi za Magharibi nchini Russia unafanyika kwa lengo la kuzusha ghasia na machafuko, kuzidisha malalamiko ya wananchi na hatimaye kutayarisha mazingira ya kufanyika mabadiliko yanayodhamini matakwa na maslahi ya Magharibi. Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na nchi za Magharibi katika uwanja huu ni kutoa misaada ya kifedha na himaya ya pande zote ya vyombo vya habari kwa wapinzani wa serikali ya Moscow na kuchafua anga ya ndani. Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla zinataka kuona Russia ikitawaliwa na mtu mwenye mielekeo na fikra za Kimagharibi kama kiongozi wa upinzani Alexey Navalny. Hata hivyo wapinzani hao wamekuwa wakifeli na kushindwa kufikia malengo yao kutokana na kuwa tegemezi sana kwa nchi za Magharibi.

Alexey Navalny akiongoza maandamano dhidi ya serikali, Moscow

Wakati huo huo Rais Vladimir Putin wa Russia anaamini kuwa, machafuko yanayotokea nchini humo yanachochewa na nchi za Magharibi kwa shabaha ya kufanyika mapinduzi ya rangi. Wamagharibi wanaona kuwa mapinduzi ya rangi nchini Russia yatapelekea kuundwa serikali yenye mielekeo ya Kimagharibi. Kwa msingi huo Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zikishirikiana na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayodai kutetea demokrasia na haki za binadamu, yamejikita zaidi katika kuchochea maandamano dhidi ya serikali ya Moscow na yanatumia vyombo vya mawasiliano ya umma kama redio na televisheni kuwachochea wananchi.

Njama hizi zinakwamishwa na mitazamo ya utaifa ya Warusi, jicho lao la shaka kwa nchi za Magharibi na umaarufu na kupendwa sana Rais Vladimir Putin baina ya raia wengi wa nchi hiyo. Licha ya hayo yote Marekani na washirika wake wa Ulaya wangali wanaingilia waziwazi mambo ya ndani ya Russia na sasa wameshikilia kisingizio cha madai ya kupewa sumu Alexey Navalny.    

Tags