Sep 07, 2020 03:35 UTC
  • Pompeo adai UAE na Israel zimeafikiana kuanzisha muungano dhidi ya Iran

Katika mwendelezo wa uchukuaji misimamo ya kiuadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amedai kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel zimefikia makubaliano ya kuanzisha muungano maalumu dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya al Mayadeen, Pompeo ameendeleza kauli zake zisizo na msingi na za kuipiga vita Iran kwa kusema: Imarati na Israel zimepata njia ya kuanzishia uhusiano ambayo inaweza kufanikisha kuundwa muungano utakaohakikisha kitisho kilichopo (Iran) hakiwezi katu kufika kwenye pwani za Marekani na hakitasababisha madhara kwa mtu yeyote yule Magharibi ya Asia.

Ukurasa wa kijamii wa Twitter wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani umemnukuu Mike Pompeo akidai kwamba: Huo ulikuwa ni wakati wa kihistoria.

Netanyahu, Trump na Bin Zayed

Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani ili kurahisisha mchakato wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel, tarehe 13 Agosti Umoja wa Falme za Kiarabu na Israel zilitangaza kuwa zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia baina yao.

Makubaliano hayo yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani..../

Tags