Sep 14, 2020 06:15 UTC
  • Onyo la Johnson kwa Umoja wa Ulaya kuhusu hatari ya kutoweka umoja wa Uingereza

Suala la kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ambalo lilianza kutekelezwa tarehe 31 Januari 2020 limekumbwa na malalamiko mengi katika maeneo yanayopigania kujitenga na nchi hiyo ya Ulaya yakiwemo ya Scotland na Ireland Kaskazini.

Huko Ireland Kaskazini, Wakristo Wakatoliki wanataka kujiunga na Jamhuri ya Ireland. Hivi sasa mzozo wa mitazamo umepamba moto baina ya Uingereza na Umja wa Ulaya kuhusu namna ya kutekelezwa suala la kujitoa nchi hiyo katika umoja huo. Huku hali ikiwa hivyo, London imedai ina wasiwasi na hatua za Umoja wa Ulaya na inahisi zitaisambaratisha na kuigawa vipande vipande Uingereza.

Waziri Mkuu wa mhafidhina wa Uingereza, Boris Johnson ametoa matamshi makali akidai kuwa Umoja wa Ulaya ni tishio kwa umoja wa ardhi ya nchi yake na amewataka wabunge wa Uingereza kupasisha mpango wake uliojaa utata. Juzi Jumamosi, Johnson aliandika katika gazeti la Daily Mail kwamba Umoja wa Ulaya unafuata siasa za misimamo mikali na zilizo tofauti kabisa na protokoli ya Ireland Kaskazini kwa lengo la kuuhamisha mpaka wa biashara wa pande mbili na kuupeleka upande wa Bahari ya Ireland. Amesema, kamwe alikuwa haamini kwamba Umoja wa Ulaya utataka kutumia makubaliano yaliyotiwa saini kwa nia njema, kuzingira baadhi ya ardhi ya Uingereza, kuimega na kuitenga na nchi hiyo. Johnson ameashiria udharura wa kuchukuliwa hatua nzito kukabiliana na juhudi za "kimaafa" za Umoja wa Ulaya za kuigawa vipande vipande Uingereza na amewataka wabunge wa nchi yake wapasishe mpango wake kuhusu namna ya kujitoa Umoja wa Ulaya licha ya kwamba mpango wake huo umejaa utata.

Brexit

 

Miezi 7 baada ya Uingereza kujitoa rasmi kwenye Umoja wa Ulaya maarufu kwa jina la Brexit, hivi sasa imebainika kwamba Brussels na London zimetumbukia kwenye mgogoro na mzozo mkubwa kuhusu utekelezaji wa Brexit hasa kuhusiana na eneo la Ireland Kaskazini. Kutokana na mwendo wa kinyonga wa utekelezaji wa Brexit haitarajiwi kwamba mchakato huo utamalizika mwaka huu licha ya kupangwa ukamilike mwishoni mwa 2020. Ndio kwanza Johnson amezuka na mpango wa kuangaliwa upya makubaliano ya Brexit likiwa ni pigo jingine katika uhusiano wa Uingereza na Umoja wa Ulaya. Sasa Johnson anataka mapatano kuhusu Ireland Kaskazini ambayo pande mbili ziliyafikia tangu mwezi Januari mwaka huu, yafumuliwe na yapangwe upya. Kwa mujibu wa mapatano hayo, mabadilishao ya bidhaa baina ya Uingereza na Ireland Kaskazini itabidi yafanyike kwa mujibu wa sheria za Umoja wa Ulaya kuanzia tarehe Mosi Januari mwaka 2021. London na Brussels zilikubaliana pia kuwa, mashirika ya kibiashara ya Uingereza yaliyoko Ireland Kaskazini nayo yafuate sheria za Umoja wa Ulaya.

Serikali ya kihafidhina ya Uingereza huko nyuma ilitangaza kwamba ilikubaliana na mpango huo kwa sababu tu ya kutaka kuondoa mgogoro na kufikia makubaliano na Umoja wa Ulaya. Sasa hatua ya hivi sasa ya Boris Johnson ya kutaka mkataba mpya kuhusu Ireland Kaskazini, inaonesha kudharau makubaliano yake ya huko nyuma na Umoja wa Ulaya na hivyo kuongeza zaidi na zaidi uwezekano wa kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya bila ya kuwa na makubaliano yoyote na umoja huo. Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umesema kuwa kitendo hicho cha Johnson ni kinyume na sheria za kimataifa na umetishia kuiwekea vikwazo Uingereza.

 

Ni jambo lililo wazi kwamba, iwapo Ireland Kaskazini itakuwa inafuata sheria za Umoja wa Ulaya, maana yake itakuwa ni kutangaza kujitenga rasmi na Uingereza. Ndio maana Boris Johnson anasema, Umoja wa Ulaya unafanya njama za kuigawa vipande vipande nchi yake. Amma cha kujiuliza ni kwamba, wakati yanafikiwa makubaliano baina ya London na Brussels ya kwamba kuanzia Januari 1, 2021, Ireland Kaskazini iwe inafuata sheria za Umoja wa Ulaya, huyu Boris Johnson na serikali yake walikuweko wapi? Je, kudai tu kwamba tulitaka kuonesha nia njema, kunatosha kuhalalisha kutia kwao ulimi puani hivi sasa na kudai makubaliano mapya? Hayo na mengineyo ni katika maswali ambayo yanamuweka pabaya mhafidhina Boris Johnson na serikali yake na ni ushahidi kwamba mgogoro wa Brexit ndio kwanza unatokota.

Tags