Sep 16, 2020 12:50 UTC
  • Kupasishwa muswada wa kuitia mkono Brexit katika Bunge la Uingereza na kiza kinene mbele ya uhusiano wa London na Brussels

Hatua ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya maarufu kwa jina la Brexit na sasa kuzusha mambo mapya, kunazidi kuingiza utata utekelezaji wa jambo hilo siku baada ya siku. Hivi sasa London imezusha mzozo mpya juu ya utekelezaji wa Brexit na kusababisha mgogoro mkubwa baina yake na Umoja wa Ulaya.

Jana Jumanne ya tarehe 14 Septemba, wabunge wa Uingereza walipasisha muswada uliowasilishwa na waziri mkuu wa nchi hiyo  Boris Johnson wa kupuuza na kutotekeleza sehemu kubwa na ya kimsingi ya vipengee vya makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya mwaka 2019 kuhusu utekelezaji wa Brexit.

Katika upigaji kura huo ambao kimsingi umefanyika kwa njia ya Intaneti kutokana na ugonjwa wa COVID-19, wabunge 340 wameupigia kura ya ndio na 263 wameupinga. Hivyo sehemu muhimu za makubaliano ya Uingereza na Umoja wa Ulaya kuhusu Brexit, zimefutwa.

Boris Johnson

Mazungumzo ya Brexit yalianza tena hivi karibuni baada ya kusitishwa kwa miezi kadhaa kutokana na kuenea kirusi cha corona. Ilikuwa inatarajiwa kupitia mazungumzo ya London na Brussels kufikiwa makubaliano katika maeneo tofauti ya kibiashara, kisiasa na kiusalama hasa suala la uchumi.

Hata hivyo hadi hivi sasa mazungumzo baina ya pande hizo mbili hayakuwa yamezaa matunda. Siku chache zilizopita, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, aliupiga jambia moyo wa mazungumzo hayo kwa kutaka makubaliano mapya tofauti na yaliyofikiwa huko nyuma hasa katika kadhia ya Ireland Kaskazini. Alisema, suala la Ireland Kaskazini ni mstari mwekundu kwa Uingereza na amewasilisha mpango mbele ya bunge la nchi hiyo ambao tayari umepasishwa; wa kufuta sehemu kubwa ya makubaliano yaliyofikiwa hadi hivi sasa baina ya pande hizo mbili. Hatua hiyo imefuta pia mapatano yaliyofikiwa kuhusu Ireland Kaskazini miezi saba iliyopita baina ya Umoja wa Ulaya na Uingereza. Kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliyofutwa na Uingereza,  ilikuwa imekubaliwa kwamba ifikapo tarehe 1 Januari 2021, eneo la Ireland Kaskazini lifuate sheria za Umoja wa Ulaya, na mashirika ya kibiashara ya Uingereza yaliyoko Ireland Kaskazini pia yalitakiwa kuanzia tarehe hiyo yafuate sheria za Umoja wa Ulaya. Sasa hivi Johnson anasema, makubaliano hayo hayafai kwani yanalenga kuimega ardhi ya nchi hiyo na kuifanya Ireland Kaskazini ijitenge na ardhi nyingine za Uingereza.

John Major, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza

Hata hivyo hatua hiyo imewakasirisha viongozi wengi ndani ya Uingereza na pia nchi za Ulaya. Nchi hizo zinaiona hatua hiyo kuwa ni sawa na Uingereza kutia ulimi puani.

David Cameron, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza ambaye ndiye yeye hasa aliyebuni Brexit anasema: Kupasishwa muswada unaoandaa mazingira ya kuvunja mkataba wa kimataifa inabidi iwe njia ya mwisho kabisa kufuatwa baada ya kushindikana njia nyingine zote.

John Major, waziri mkuu mwingine wa zamani wa Uingereza kutoka chama cha Wahafidhina anasema, mpango wenye utata mwingi wa serikali ya Johnson unadhoofisha itibari ya Uingereza kimataifa na inaionesha dunia kuwa Uingereza haina mwamana na ni kigeugeu.

Viongozi wa nchi nyingine za Ulaya pia wanasema, jaribio hilo la Uingereza la kudharau makubaliano yaliyofikiwa kimataifa, ni kwenda kinyume na ada za kimataifa na hawawezi kukivumilia kitu kama hicho. Bunge la Ulaya limeonya kwamba kamwe halitopasisha mikataba ya kibiashara na Uingereza. 

Ofisi za Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji

 

Kipindi cha mpito cha uhusiano baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya ambacho kilikubaliwa kiendelee kuchunga sheria za kabla ya Brexit, kinamalizika mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu wa 2020. Wakati muda huo ukikaribia kumalizika, Uingereza imezusha mgogoro mpya katika utekelezaji wa Brexit. London imetangaza kuwa, kama Umoja wa Ulaya hautoafiki inayoyataka, basi itajitoa kwenye umoja huo bila ya kufikia makubaliano yoyote nao, suala ambalo bila ya shaka litakuwa ni pigo kubwa kwa uchumi wa nchi za Ulaya ikiwemo Uingereza yenyewe. Hilo litakuwa ni pigo pia katika uhusiano wa kisiasa wa pande hizo mbili. Ikumbukwe kuwa, mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2021, sheria za Shirika la Kimataifa la Biashara zitaanza kutekelezwa katika uhusiano wa kibiashara wa Uingereza na Umoja wa Ulaya. Inaonekana kwamba kama hali itaendelea hivi hivi ilivyo hivi sasa, basi mchakato wa Brexit ndio utakaokuwa ukomo wa ndoto za London kuhusu kufaidika na uamuzi wake wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya.

Tags

Maoni