Sep 17, 2020 02:21 UTC
  • Trump: Nilitaka kumuua Rais wa Syria lakini Mattis alinizuia

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema kuwa, kitendo cha rais wa Marekani, Donald Trump cha kukiri hadharani kwamba alikuwa na nia ya kumuua Rais Bashar al Assad wa Syria kinaonesha jinsi dola hilo la kibeberu linavyotumia kila unyama ikiwa ni pamoja na kuyatumia magenge ya kigaidi kufikia malengo yake.

Katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya Fox News hivi karibuni, rais wa Marekani, Donald Trump alikiri kwamba alikuwa na nia ya kumuua Rais Bashar al Assad wa Syria lakini James Mattis, waziri wa ulinzi wa wakati huo wa Marekani, alimzuia.

Shirika rasmi la habari la Syria (SANA) limeinukuu Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ikijibu ujuba huo wa Donald Trump na kusisitiza kuwa, kukiri huko Trump kunaonesha jinsi watawala wa Marekani wasivyo na maadili na jinsi walivyoporomoka chini kibinadamu.

Rais Bashar al Assad wa Syria

 

Wizara ya Mambo ya Nje wa Syria imeongeza kuwa, Trump anazidi kuonesha kuwa mfumo wa utawala nchini Marekani ni wa maharamia na majambazi ambao hawasiti kufanya jinai yoyote ile kufikia malengo yao haramu.

Taarifa ya wizara hiyo pia imesema, kukiri rais wa Marekani kwamba alikusudia kumuua kigaidi Rais Bashar al Assad; rais wa nchi huru, mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni uthibitisho mwingine kwamba serikali ya Marekani ni serikali isiyojali kabisa sheria. Ni serikali ambayo inafanya mauaji na ugaidi wa kiserikali na jinai nyingine nyingi bila ya kujali sheria za kimataifa, wala ubinadamu na wala maadili.

Tags

Maoni