Sep 17, 2020 13:03 UTC
  • Mazungumzo ya Wafghani yaendelea Doha, Taliban yakataa ombi la serikali la kusitisha vita

Msemaji wa ofisi ya kisiasa ya kundi la Taliban nchini Qatar amelikataa ombi la serikali ya Afghanistan la kusitisha vita, wakati pande hizo mbili zinaendelea na mazungumzo ya amani katika mji mkuu wa Qatar, Doha.

Muhammad Naeem Wardak amesema:  "Haiingii akilini tuhitimishe ndani ya muda wa saa moja vita ambavyo vimechukua muda wa miaka 20; kwa maoni yetu, inapasa ichunguzwe kwanza sababu ya vita hivi kisha ndipo usitishaji vita wa kudumu utekelezwe."

Sambamba na kusisitiza msimamo wa kundi la Taliban wa kutatua tofauti zilizopo baina yake na serikli ya Afghanistan, Wardak ameongeza kuwa, kundi lao linataka uasisiwe utawala wa Kiislamu katika nchi hiyo.

Hayo yanajiri wakati Nader Naderi, msemaji wa ujumbe wa wawakilishi wa serikali ya Afghanistan katika mazungumzo na kundi la Taliban alitangaza jana Jumatano katika siku ya tano ya mazungumzo hayo, kwamba ajenda za mazungumzo zinakaribia kukamilika na wajumbe wa pande mbili wanakubaliana juu ya masuala mengi.

Wawakilishi wa Taliban katika mazungumzo ya amani Doha

Naderi ameongeza kuwa, mazungumzo hayo yataendelea hadi utakapofikiwa mwafaka uliokusudiwa.

Katika mazungumzo hayo ya kutafuta suluhu na kurejesha amani nchini Afghanistan, serikali ya Kabul na kundi la Taliban zinajadiliana kuhusu kutekeleza usitishaji vita, mfumo ujao wa kisiasa wa Afghanistan, mgawanyo wa madaraka na namna ya kuwaunganisha wanamgambo wa Taliban katika vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo.../

Tags

Maoni