Sep 18, 2020 12:12 UTC
  • Tahadhari ya UN kuhusu mgogoro wa njaa, zaidi ya watu milioni 30 wanakabiliwa na kifo

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kuwa watu milioni 30 kote duniani wanakabiliwa na kifo kutokana na baa kali la njaa na wanahitajia misaada ya kibinadamu.

Mkurugenzi wa WFP, David Beasley amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba sababu ya hatari ya kifo inayowakabili watu milioni 30 katika maeneo mbalimbali ya dunia ni vita, mapigano, mabadiliko ya hali ya hewa, changamoto na matatizo yaliyosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.

David Beasley ameongeza kuwa, karibu watu milioni 270 kote duniani wanasumbuliwa na utapiamlo na wanakaribia kutumbukia katika ukata wa kupindukia. 

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, vita vya Saudi Arabia na washirika wake nchini Yemen vimeifanya thuluthi mmoja na raia wa nchi hiyo kukosa mahitaji yao ya chakula.

Tarehe 5 mwezi huu wa Septemba pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitahadharisha kuhusu hatari ya njaa na ukosefu wa chakula nchini Yemen na nchi tatu za Afrika ambazo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Niger na Sudan Kusini.

UN: Mamilioni ya Wayemeni wanasumbuliwa na njaa

Yemen ilivamiwa na Saudi Arabia na washirika wake wakisaidiwa na Marekani mwezi Machi mwaka 2015 na maelfu ya raia wa nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na uvamizi huo. 

Vita vya Saudia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen vimeitumbukiza nchi hiyo katika umaskini mkubwa na uhaba wa chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu. 

Maoni