Sep 19, 2020 04:27 UTC
  • Tarehe 20 Septemba; Marekani kupata pigo jingine?

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hakuna kitu kipya kitakachotokea kesho tarehe 20 Septemba na kwamba, inamtosha kwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kulisoma azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Dakta Muhammad Javad Zarif ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter sambamba na kukaribia siku ya Marekani kutoa tangazo kwa ajili ya kurejeshwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kwamba: Mike Pompeo anakosea, Marekani siyo mwanachama tena wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na utaratibu wa kurejesha vikwazo siyo jambo jepesi bali ni tata na kitu cha muda mrefu.

Baada ya Marekani kushindwa mwezi uliopita kupasisha azimio dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokuwa na lengo la kuendelea kubakishwa vikwazo vya silaha dhidi ya ran, imechukua hatua ya upande mmoja na ikitumia vitisho inafanya njama kuhakikisha kwamba, vikwazo vyote dhidi ya Iran vinarejeshwa kwa kutumia mchakato unaofahamika kama 'Snapback Mechanism' ‘utaratibu wa papo kwa hapo’ na kivitendo iyasambaratishe makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

 

Katika hali ambayo Marekani ina tafsiri yake kuhusiana na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kimsingi yenyewe si mwanachama tena wa makubaliano hayo hata iwe na fursa hiyo ya kutoa tafsiri iitakayo; na pili ni kuwa, azimio hilo si jambo la kando na makubaliano ya JCPOA. Hivyo katika mazingira kama haya, hatua zote za Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni za kimabavu na zilizo kinyume cha sheria.

Mikhail Ulyanov, balozi wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao yake mjini Vienna Austria amezungumzia harakati za Marekani za kutaka kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran na kusema kuwa: Hakuna mtu yeyote anayezipa umuhimu juhudi za kuchekesha za Marekani za kutaka kujionyesha kwamba, ni mshirika aliyejitangaza mwenyewe katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia Mei 2018, kimsingi nchi hiyo siyo mshirika tena wa makubaliano hayo hata iwe na haki ya kutaka kutumia utaratibu ulioainishwa ndani ya makubaliano hayo kupitia azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Akthari ya nchi wanachama wa Baraza la Usalama mwezi Agosti uliopita zilipinga azimio dhidi ya Iran lililokuwa limependekezwa na Marekani na hivyo kusajiliwa pigo la kihistoria dhidi ya Washington katika Umoja wa Mataifa.

Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kusimama kidete dhidi ya hatua za upande mmoja za Marekani kunadhamini mfumo wa kimataifa uliopo kwa ajili ya kudhamini amani na usalama wa dunia. Hapana shaka kuwa, kulegeza kamba au kupuuza hatua haribu za utawala wa kibeberu wa Marekani kutakuwa na matokeo mabaya kwa mataifa yote na siyo kwa mataifa kadhaa tu.

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anaamini kuwa, ili kuyabakisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mkabala na hatua za uchukuaji maamuzi ya upande mmoja za Marekani, wanachama wote wa Baraza la Usalama wana azma moja na hawapaswi kuruhusu Washington iyatwishe mataifa mengine matakwa na irada yake, na hivyo  kuyasambvaratisha makubaliano ya JCPOA yanayoungwa mkono kimataifa na ambayo yameidhinshwa pia na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

 

Kwa kuzingatia irada na azma iliyopo katika anga ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wanachama na mwenyekiti wake wanapinga tafsiri inayotolewa na Marekani kuhusiana na azimio 2231 la baraza hilo na kwa msingi huo kesho Septemba 20 hakutatokea kitu kipya kwa maslahi ya Marekani, isipokuwa kama vitisho na mashinikizo ya Marekani yatakuwa na taathira na hivyo kubadilisha hali na msimamo wa sasa wa nchi wanachama katika taasisi hiyo.

Aal kulli haal, kukabiliana na hatua za upande mmoja za Marekani na Iran kupata haki zake zilizoainishwa katika JCPOA ndiyo sharti la kubakia makubaliano hayo na kwamba, hatua yoyote ile ya kuwa pamoja na Washington katika Baraza la Usalama maana yake ni kudhoofisha misimamo ya pande kadhaa na hilo litakabiliwa na radiamali mwafaka kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags

Maoni