Sep 19, 2020 07:39 UTC
  • Troika ya Ulaya: Hatua yoyote ya kuirejeshea vikwazo Iran ni kinyume cha sheria

Nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa ambazo ni maarufu kwa jina la Troika ya Ulaya kwa mara nyingine zimepinga njama za Marekani za kutaka kuirejeshea Iran vikwazo vilivyoondolewa na Umoja wa Mataifa baada ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika barua yao ya jana Ijumaa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, nchi hizo tatu za Ulaya zilisisitiza kwamba kusimamishwa vikwazo vya Iran kutaendelea hata baada ya tarehe 20 Septemba na kwamba uamuzi au hatua yoyote ya kuirejeshea vikwazo Iran ni kinyume cha sheria.

Katika barua yao hiyo, nchi za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa kwa mara nyingine zimesisitiza kuwa zitaendelea kuwemo kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Baada ya kushindwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani imedai kuwa itavirejesha yenyewe vikwazo vya umoja huo dhidi ya Iran licha ya kwamba si mwanachama tena wa JCPOA.

Nchi zilizobakia ndani ya JCPOA

 

Tarehe 20 mwezi uliopita wa Agosti, Marekani ilitoa tangazo mbele ya Baraza la Usalama ikidai kuwa Iran haikuheshimu mapatano hayo hivyo vikwazo vya Umoja wa Mataifa vitarejea vyenyewe dhidi ya Tehran ifikapo kesho tarehe 20 Septemba. Hata hivyo jambo hilo nalo limepingwa vikali na wajumbe wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hivi karibuni pia nchi tatu za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na China na Russia zilitoa tamko la pamoja na huku zikigusia kitendo cha Marekani cha kujitoa kijeuri kwenye mapatano hayo zilisisitiza kuwa, Washington haina haki yoyote ya kuirejeshea vikwazo Iran kwa kutumia azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama lililopasisha mapatano ya JCPOA kwani si mwanachama tena wa makubaliano hayo.

Maoni