Sep 19, 2020 12:49 UTC
  • Ufaransa yakadhibisha madai ya Marekani dhidi ya Hizbullah

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imesema hakuna ushadidi wowote unaoonyesha kuwa tawi la kijeshi la harakati ya Hizbullah ya Lebanon limefanya magendo ya kemikali kwa ajili ya kutengeneza mada za mlipuko nchini Ufaransa, kama inavyodai Marekani.

Agnes von der Muhll, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa akijibu madai hayo yaliyotolewa na Washington katika kikao na waandishi wa habari siku ya Ijumaa amesema, "kwa ufahamu wetu, hakuna ushahidi wowote wenye mashiko wa kuthibitisha madai hayo nchini Ufaransa hii leo."

Siku ya Alkhamisi, Nathan Sales, Mratibu wa Vita dhidi ya Ugaidi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alidai kuwa, Hizbullah imekuwa ikifanya magendo ya kemikali ya 'Ammonium nitrate' katika nchi za Ulaya za Ufaransa, Ubelgiji, Ugiriki, Italia, Uhispania na Uswisi tokeo mwaka 2012.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Marekani alidai kuwa, Hizbullah ina shehena za kemikali hiyo hatari katika nchi hizo za Ulaya kwa shabaha ya kuunda mada za milipuko na kutekeleza mashambulizi ya kigaidi kwa eti kwa niaba ya Iran. 

Rais Macron katika ziara yake ya kukagua bandari ya Lebanon iliyoripuka

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ambaye mapema mwezi huu alifanya safari kwa mara ya pili ya kuitembelea Lebanon tangu ilipotokea miripuko katika bandari ya Beirut tarehe 4 Agosti alisema Hizbullah ni mwakilishi wa sehemu mojawapo ya wananchi wa Lebanon.

Alisisitiza kuwa, Hizbullah ni mwakilishi wa sehemu mojawapo ya wananchi wa Lebanon na ni chaguo la wananchi hao na kuna ushirika kati ya Hizbullah na vyama vingine.

Tags

Maoni