Sep 20, 2020 02:40 UTC
  • Matarajio ya nchi wanachama kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)

Utumiaji wa nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani ni haki ya wanachama wote wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo swali linaloulizwa ni kwamba, je, haki hiyo inalindwa na kutekelezwa ipasavyo? Na kama kuna tatizo katika uwanja huo, sababu yake ni nini?

Suala hili linaweza kuchunguzwa kwa mitazamo miwili tofauti. Mtazamo wa kwanza ni wa kuwa na imani kamili na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, na kwa msingi huo hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu shughuli na utendaji wa majukumu ya wakala huo. Mtazamo mwingine ni ule unaotilia shaka suala la kujitawala na kujitegemea wakala wa IAEA katika utendaji wa kazi na shughuli zake. Jambo linaloibua mtazamo huu ni mienendo ya kindumakuwili inajitokeza mara kwa mara katika ripoti za wakala wa IAEA au jinsi wakala huo unavyofumbia macho harakati zisizo za kawaida za masuala ya nyuklia katika baadhi ya nchi. Suala hili limebainishwa na kuwekwa wazi katika hotuba ya mwakilishi wa Iran katika kikao cha msimu cha Baraza la Magavana wa wakala wa IAEA mjini Geneva.

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika ofisi ya Umoja wa Mataita mjini Geneva, Kazem Gharib Abadi alishiria wasiwasi uliopo katika uwanja huo na kutoa mfano kwa kuzungumzia jinsi utawala haramu wa Israel ulivyopata kwa siri silaha za nyuklia na unavyopuuza na kukanyaga sheria na kanuni zote za kimataifa; suala ambalo linatishia usalama na amani ya kimataifa.

Kazem Gharib Abadi, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika ofisi ya UN mjini Geneva  

Mwakilishi wa Iran katika jumuiya za kimataifa mjini Geneva pia ameashiria kufichuliwa baadhi ya shughuli za siri za nyuklia za Saudi Arabia na ameutaka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na Baraza la Magavana wa wakala huo kuhakikisha kwamba, Saudi Arabia inaheshimu majukumu yake kwa majibu wa hati na kanuni za IAEA.

Gharib Abadi ameashiria hatua ya Saudi Arabia ya kukaidi kutekeleza kikamilifu makubaliano na manuni za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kimya cha nchi ambazo daima zimekuwa zikieleza wasiwasi wao kuhusu suala la kutekelezwa sheria na kanuni hizo.

Ni vyema kusema hapa kuwa licha ya kwamba Saudia ni mwanachama katika Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia (NPT) lakini hadi sasa imekataa kuwaruhusu wasimamizi wa wakala wa IAEA kukagua shughuli zake za nyuklia. Ripoti iliyotolewa siku zilizopita na Kongresi ya Marekani ilifichua kuwa, serikali ya rais wa nchi hiyo, Donald Trump, inaharakisha mwenendo wa kuipatia Saudi Arabia teknolojia nyeti sana ya nyuklia. 

Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia (NPT)

Mtandao wa uchambuzi wa habari za kiulinzi wa Defense News umeripoti kuwa: "Sera kama hizi zilipelekea baadhi ya nchi kutengeneza silaha za nyuklia kwa msaada wa Marekani. Saudi Arabia pia imeweka mguu katika njia hii."

Hapana shaka kwamba kupuuza masuala haya kunatishia usalama na amani ya kikanda na kimataifa, kutatiza kazi ya kudhibiti silaha na kutoa changamoto kwa muundo wa sasa wa kupokonya na kuharibu silaha za maangamizi ya umati. 
Ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi, nchi wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zinatarajia kuwa, wakala huo utatoa ripoti zisizopendelea upande wowote na za kujitegemea kuhusu maswali kwamba, vipi, kwa nini, kwa kiwango gani na nchi gani inakwamisha utendaji wa wakala huo wa kimataifa na kuiwasilisha ripoti hiyo kwa nchi wanachama.   

Maoni