Sep 20, 2020 07:19 UTC
  • Biden amtaka Trump ang'atuke madarakani

Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrat amemtaka rais wa nchi hiyo Donald Trump ang'atuke madarakani kwa sababu ya uongozi mbovu alioonyesha katika kukabiliana na virusi vya corona.

Joe Biden ameyasema hayo alipowahutubia wananchi wa jimbo la Pennsylvania na akaeleza kwamba, Trump ndiye anayebeba dhima ya kila anayepoteza maisha ndani ya Marekani kwa sababu ya kuambukizwa virusi vya corona.

Biden ameongeza kuwa: "Laiti kama rais angetimiza wajibu wake tokea awali, watu wote waliopoteza roho zao, leo wangekuwa hai."

Mgombea huyo wa urais wa Marekani katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 3 amesema, hakuna kitu kingine chochote anachokipa umuhimu Trump zaidi ya soko la hisa na uchaguzi; na akamkosoa vikali kiongozi huyo na kumtaka aondoke madarakani.

Baada ya kupungua kwa majuma kadhaa, maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha maradhi ya Covid-19 yameongezeka tena nchini Marekani.

Nchi hiyo ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu walioaga dunia na walioambukizwa virusi vya corona duniani kote, ambapo kwa mujibu wa takwimu rasmi, hivi sasa idadi ya walioambukizwa virusi hivyo imeshafika watu milioni saba na waliofariki dunia wameshapindukia 203,000.

Serikali ya Washington, na hasa rais Donald Trump mwenyewe amekuwa akikosolewa na kulaumiwa vikali kwa kutowajibika ipasavyo katika kukabiliana na mripuko wa janga la corona lililoikumba dunia nzima.../

Tags

Maoni