Sep 20, 2020 11:34 UTC
  • Pigo jingine kubwa kwa Marekani; UN, EU, Troika zaikana tena Washington

Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU) na nchi tatu kubwa za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinazojulikana kwa jina maarufu la Troika ya Ulaya kwa mara nyingine tena zimeikana Marekani na kusema kuwa madai yake ya kurejea vyenyewe vikwazo vya Iran hayana msingi wowote wa kisheria.

Akitoa msimamo wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa umoja huo, António Guterres amesema, UN haiwezi kuchukua hatua yoyote ya kurejesha vikwazo vya Iran kutokana na kukosekana ushahidi wa maana wa kuthibitisha madai ya Marekani kuhusu suala hilo.

Ikumbukwe kuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo amedai kuwa eti vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vikiwemo vya silaha, vimerejea vyenyewe.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi tatu za Ulaya za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zimetoa tamko la pamoja na kusema kuwa zitaendelea kuheshimu azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA na hazitojali madai ya Marekani inayodai kuwa vikwazo hivyo vimerejea vyenyewe. 

Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani

 

Kabla ya hapo pia mwakilishi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa alikuwa ametoa tamko na kusema, vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran havipo tena, vimeshaondolewa na Umoja wa Mataifa na hali hiyo itaendelea vivyo hivyo kwani nchi tatu za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zinaendelea kuheshimu mapatano ya JCPOA. 

Kwa upande wake, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuhusu madai hayo yasiyo na mashiko ya Marekani kwamba EU itaendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA na itaendelea kuhesabu kuwa vikwazo dhidi ya Iran vimeshaondolewa.

Josep Borrell amesema hayo leo Jumapili katika tamko rasmi na kuongeza kuwa, kitendo cha Marekani cha kujitoa katika mapatano ya JCPOA kimempokonya haki zote za kutumia vipengee vya makubaliano hayo.

Maoni