Sep 21, 2020 10:33 UTC
  • Msimamo mmoja wa kundi la 4+1 mbele ya madai hewa ya Marekani kuhusu Iran

Licha ya Marekani kutoa madai hewa ya kuanza kutekelezwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran kuanzia jana Jumapili Septemba 20, 2020 vikiwemo vikwazo vya silaha, lakini mataifa ya dunia yamepinga madai hayo ya Washington na yamechukua msimamo imara kiasi kwamba inaonekana kama vile hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea.

Wajumbe wa kambi za Mashariki na Magharibi za kundi la 4+1 linaloundwa na wapinzani na waitifaki wa Washington, wote wamechukua msimamo mmoja wa kuipinga Marekani katika suala hilo. Zhang Jun, mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa na Vassily Nebenzia mwakilishi wa kudumu wa Russia katika umoja huo wameliandikia barua Baraza la Usalama na kusisitiza kuwa, hatua ya Marekani ya eti kuanza kutekeleza vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran maarufu kwa jina la "Snapback Mechanism," ni kinyume cha sheria na kwamba vikwazo vya Iran vilivyoondolewa na Umoja wa Mataifa baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA vitaendelea kuondolewa. Mwakilishi huyo wa Russia katika Umoja wa Mataifa ameishutumu Marekani kwa hatua yake hiyo na kusema kuwa, inaumiza sana kuona nchi yenye ukubwa wote huu inajidhalilisha kiasi chote hiki na inafanya ubishi wa kuchupa mipaka wa kupingana kupindukia na ya wajumbe wengine wa Baraza la Usalama.

Wakuu wa Troika ya Ulaya

 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi tatu za Ulaya maarufu kwa jina la Troika ya Ulaya  yaani Uingereza, Ujerumani na Ufaransa ambao ni wajumbe wengine wa kundi la 4+1 licha ya kwamba ni waitifaki wa jadi ya Marekani, lakini sasa hivi kutokana na siasa mbovu za Washington wamechukua msimamo imara wa pamoja wa kuipinga nchi hiyo ya kibeberu. Katika tamko lao la pamoja, mawaziri hao wamesisitiza kuwa wataendelea kuheshimu azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha mapatano ya JCPOA na hazishughulishwi na madai ya Marekani ya kuanza utekelezaji wa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran. Katika tamko lao hilo, nchi hizo tatu za Ulaya zimesema kuwa, kwa vile Marekani ilijitoa yenyewe (tena kijeuri) katika makubaliano ya JCPOA hapo tarehe 8 Mei 2018, sasa hivi nchi hiyo si mwanachama tena wa mapatano hayo kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha azimio nambari 2231 lililoanza kutekelezwa mwaka 2015. Wamesema kwa mujibu wa kifungu hicho, Marekani haina haki tena ya kutumia vipengee vya makubaliano hayo, hivyo madai yake ya kutumia mfumo wa "Snapback Mechanism" kuirejeshea vikwazo Iran hayana msingi wowote wa kisheria.

Msimamo huo imara wa Troika ya Ulaya ni pigo jingine kubwa kwa serikali ya Donald Trump huko Marekani ambayo ilikuwa na tamaa ya angalau kupata uungaji mkono wa japo kunyamaza kimya tu waitifaki wake hao wa jadi wa Ulaya. Huku kusema kweli ni kutengwa kubaya kimataifa ambako hakujawahi kuikumba Marekani katika historia yake isipokuwa hivi sasa wakati wa utawala wa Donald Trump.  Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani ameshindwa kuonesha hamaki zake kutokana na msimamo huo wa nchi za Ulaya; amezishambulia kwa maneno na kutoa vitisho vya kuziwekea vikwazo. Katika tahariri yake, gazeti la New York Times limeandika: Hatua ya nchi za dunia zikiwemo za waitifaki wa karibu kabisa wa Marekani barani Ulaya ya kuipinga Washington. ni suala ambalo linaonesha kutengwa vibaya Marekani, kimataifa. 

Donald Trump, rais wa Marekani aliyevurunda kila sehemu

 

Hata hivyo, serikali ya watu waliojaa kiburi na ubishi huko Marekani tangu hapo zamani haikutarajiwa kunyamaza kimya, bali itafanya kila iwezalo kuonesha kuwa haijafeli. Hii ni kusema kuwa,  katika hatua nyingine yenye lengo la kuivuruga zaidi dunia, rais wa Marekani, Donald Trump amekusudia kutangaza siku ya Jumatatu, amri ya utekelezaji wa vikwazo dhidi ya Iran na kupewa adhabu, yeyote atakayepinga amri hiyo ya Marekani. Wizara ya Hazina ya Trump iko mbioni kuainisha vikwazo na adhabu zitakazotolewa. Lakini kilicho wazi ni kwamba, sasa Trump hakabiliani na Iran pekee, bali anakabiliana na dunia nzima. Kwani msimamo mmoja imara wa kundi la 4+1 linaloundwa na nchi kubwa duniani za Russia, China, UIngereza, Ufaransa, Umoja wa Ulaya pamoja na Ujerumani umeonesha kuwa kundi hilo haliko tayari kufuata kibubusa siasa za kibeberu za Marekani. Wachambuzi wa mambo wanasema, si jambo rahisi kwa Marekani kufikia ndoto yake hiyo iliyojengwa na madai hewa. Katika uchambuzi wake wa kina, gazeti la Washington Post limegusia kupungua heshima ya Marekani duniani na kuandika: Trump ametoa pigo kubwa sana kwa heshima na itibari ya Marekani ulimwenguni. Kwa upande wake, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya Marekani isifanye mambo ambayo yatazidi kuiaibisha. Rais Rouhani amesema, Iran, kamwe haiwezi kukubali kuburuzwa.

Tags

Maoni