Sep 23, 2020 01:34 UTC
  • Russia kuendelea kushirikiana kijeshi na Iran licha ya vikwazo vya Marekani

Seneta mmoja wa Russia amesema nchi hiyo itaendelea kuwa na ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa kijeshi licha ya uhasama, vikwazo na mashinikizo ya Marekani.

Vladimir Dzhabarov ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza la Seneti la Russia amesema hayo na kuongeza kuwa, Russia itaendelea kuwa na ushirikiano wa kiufundi na Iran katika uga wa kijeshi licha ya dikrii iliyotolewa na Rais Donald Trump ya kutaka 'kuadhibiwa kwa vikwazo' nchi zitakazoziuzia Iran silaha baada ya marufuku ya silaha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufikia tamati karibuni hivi.

Ameeleza bayana kuwa, tayari Marekani imeziwekea nchi mbili hizi vikwazo vingi na kwamba vikwazo hivyo vipya havitakuwa na taathira yoyote katika uhusiano wa kiulinzi wa Moscow na Tehran.

Seneta huyo wa Russia ameongeza kuwa, inasikitisha namna Marekani inavyotumia sera zake za mabavu kuziburuza nchi nyingine duniani zifuate misimamo na mienendo yake, na kujiona kuwa ina nguvu zaidi hata kuliko Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Uhusiano wa Iran, Russia na China umezidi kuimarika licha ya vikwazo vya miaka mingi vya US

Siku ya Jumatatu pia, Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisema vitisho vya kutumia vikwazo katu haviwezi kusimamisha ustawi wa ushirikiano wa kiulinzi wa Tehran na Moscow.

Ryabkov alisema hayo katika mahojiano na shirika la habari la TASS na kuongeza kuwa, "Hatuogopi vikwazo vya Marekani kwani tumeshavizoea. Marufuku ya silaha ya Washington hayawezi kuvuruga kivyovyote sera yetu ya kushirikiana na Iran katika uga wa kijeshi.

 

Tags

Maoni