Sep 23, 2020 08:07 UTC
  • Emmanuel Macron
    Emmanuel Macron

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amekiri kuwa, sera ya mashinikizo ya juu zaidi ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imegonga mwamba.

Rais Macron amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo pia amepuuzilia mbali jitihada za Marekani za kutaka kurejeshwa upya vikwazo vya UN dhidi ya Tehran.

Amesema: Stratejia ya mashinikizo ya juu zaidi ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa miaka kadhaa sasa, imeshindwa kutamatisha eti hatua zinazoyumbisha uthabiti za Iran katika eneo au kuhakikisha kuwa Tehran haiundi silaha za nyuklia, ndiposa Ufaransa pamoja na washirika wake Ujerumani na Uingereza wanataka kuendelea kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya Vienna ya mwaka 2015.

Macron amebainisha kuwa, Marekani ilijiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa na kwa msingi huo haina haki wala kibali cha kurejesha vikwazo vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baraza la Usalama la UN limepinga njama mara mbili njama za US dhidi ya Iran ndani ya wiki chache zilizopita

Rais wa Ufaransa amesisitiza kuwa, Ufaransa haiwezi kuthubutu kuchukua hatua ya upande mmoja ya kuhuisha utaratibu wa vikwazo vya UN dhidi ya Iran, mchakato ambao Marekani yenyewe ambayo imejiondoa kwenye JCPOA haiwezi kuutekeleza.

Siku ya Jumatatu, Marekani ilitangaza vikwazo vipya dhidi ya Wizara ya Ulinzi ya Iran ili kutaka kuonyesha kuwa vikwazo vya UN dhidi ya Iran vimerejeshwa upya, hatua ambayo imekosolewa na Russia. China na wadau wengine wa JCPOA.

Tags

Maoni