Sep 24, 2020 02:41 UTC
  • Sababu za kufifia matukio ya Asia Magharibi katika mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaendelea kufanyika mwaka huu katika hali ambayo, matukio ya eneo la Asia Magharibi yamefifia na kutoakisiwa sana katika hotuba za viongozi waliohutubia katika siku ya kwanza ya mkutano huo.

Mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa una tofauti kubwa na mikutano ya hapo kabla ya umoja huo. Kwa mara ya kwanza viongozi wa mataifa wanahutubia mkutano huo kwa njia ya mawasiliano ya intaneti na hotuba zao zinarushwa baada ya kuwa zimerekodiwa. Hilo limetokana na mazingira ya sasa ynayotawala ulimwenguni ya kuenea virusi vya corona. Kwa muktadha huo, mara hii hakutakuwa na mikutano ya kando kando ya mazungumzo baina ya viongozi mbalimbali pambizoni mwa mkutano huo.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Marais Xi Jinping wa China, Donald Trump wa Marekani, Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Vladimir Putin wa Russia, Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Emannuel Macron wa Ufaransa ni miongoni mwa viongozi na shakhsia muhimu ambao hutuba zao zilirushwa hewani katika siku ya kwanza ya mkutano huo.

Kutokana na kuenea kote ulimwenguni virusi vya corona ni jambo la kawaida kuona kuwa moja ya maudhui za hotuba za viongozi hao ni kuhusiana na janga hili la Covid-19. Kinyume na miaka ya nyuma, mara hii, matukio ya eneo la Asia Magharibi hayajawa mhimili mkuu wa hotuba za viongozi katika mkutano huu. Ndio maana katika hotuba zilizorushwa hewani siku ya kwanza ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, matukio ya Asia Magharibi hayakuakisiwa pakubwa ikilinganisha na miaka ya huko nyuma.

Rais Vladimir Putin wa Russia akihutubia katika mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

 

Sababu ya kwanza ya jambo hilo ni kuwa, kiwango cha migogoro ya kiusalama katika eneo husika kimepungua kwa sasa. Mgogoro wa Syria ukilinganishwa na miaka ya huko nyuma, hivi sasa umepungua na kunashuhudiwa katika nchi hiyo usalama na uthabiti wa kiwango fulani. Kivitendo kundi la kigaidi la Daesh limo katika hali ya kusambaratika kabisa na kuna mabaki ya wapiganaji wachache ambao wanaendesha harakati zao za hapa na pale katika baadhi ya nchi zaAsia Magharibi.

Vita vya kidhulma dhidi ya Yemen vingali vinaendelea, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, kukomesha vita hivi siyo jambo ambalo linapewa kipaumbele na madola yenye nguvu na hata Umoja wa Mataifa. Licha ya kuwa, maafa ya kibinadamu yanaendelea kusambaa katika eneo la Asia Magharibi, hususan hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa nchini Yemen na hata huko Syria, lakini utendaji wa madola makubwa ulimwenguni unaonyesha kuwa, kimsingi suala la haki za binadamu halina nafasi katika mfumo wa sasa wa dunia.

Sababu ya pili ya kufifia matukio ya Asia Magharibi katika hotuba za viongozi wa dunia kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu ni kuwa, mfumo wa dunia hivi sasa unakabiliwa na mambo makubwa zaidi katika hali ya hivi sasa. Hatua za Marekani za kujichukulia maamuzi kiholela, kupuuzwa sheria za kimataifa, kudhoofisha Umoja wa Mataifa na kushadidi vita baridi baina ya madola makubwa duniani ni miongoni mwa mambo makubwa ambayo ni tishio kwa sasa na yanayoukabili mfumo wa ulimwenguni hivi sasa.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

 

Ni kwa muktadha huo, ndio maana Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akaitaka dunia katika hotuba yake ijiepushe na vita baridi vipya na kusema kuwa: Kutokana na kuweko maradhi yaliyoenea kila mahala ya Covid-19, ulimwengu unahitajia usitishaji vita, kuzima moto wa migogoro na mizozo na hivyo kuzuia kutokea tena vita baridi.

Kimsingi ni kuwa hii leo, daghadagha na hangaiko kuu la viongozi wa madola makubwa ya dunia na katika eneo hili ni kuzuia kusambaratisha mfumo wa dunia na kuzuia pia kudhoofishwa nafasi ya nchi zao katika mfumo wa ulimwengu. Wasiwasi huu chimbuko lake ni utendaji wa kindumakuwili na kibabe wa serikali ya sasa ya Marekani. Rais Xi Jinping wa China ameashiria katika hotuba yake juu ya kupenda ukubwa Marekani na kujiona iko juu ya mataifa mengine. Kwa upande wake, Rais Vladimr Putin wa Russia ameashiria katika hotuba yake hatua za kudhoofisha asasi za kimataifa hususana Shirika la Afya Duniani (WHO).

Pamoja na hayo, ukosoaji wa wazi kabisa ni ule uliobainishwa na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika hotuba yake, Rais Rouhani amekosoa wazi kabisa suala la  Marekani kujichukulia maamuzi kivyake pamoja na ubabe wake katika mfumo wa dunia na kusema kuwa, zama za ubeberu na mamlaka ya dola moja kutoa amri kwa madola mengine zimefikia tamati na akafafanua kuwa: Kutoa mara mbili Baraza la Usalama tamko la wazi la "hapana" kwa Marekani kwa sababu ya kutaka kulitumia kimaslahi na kinyume cha sheria baraza hilo na azimio nambari 2231 ni ushindi si kwa Iran tu bali kwa zama za mfumo wa kimataifa katika ulimwengu wa baada ya enzi za Magharibi ambapo utawala unaojinadi kuwa na mamlaka ya kuamuru unazama kwenye shimo la kutengwa ulilojichimbia wenyewe.

Tags

Maoni