Sep 24, 2020 08:10 UTC
  • Mivutano baina ya Marekani na China yashadidi baada ya hotuba ya Trump katika Umoja wa Mataifa

Katika hotuba yake ya mwisho kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kipindi chake cha kwanza cha urais wa Marekani, Donald Trump amejikita zaidi katika masuala ya China na Iran na kudai kuwa, Marekani imejiondoa katika makubaliano mabaya sana ya nyuklia ya JCPOA na imeiwekea Iran vikwazo vya kulema.

Katika hotuba hiyo kali pia Trump amekariri tena kwamba, virusi vya corona ni "virusi vya Kichina". Trump alisema Marekani inapambana na adui asiyeonekana (virusi vya Kichina) na kuongeza kuwa, China ambayo ndiyo iliyoeneza virusi vya corona inapaswa kuwajibishwa na kukalishwa kiti moto.

Katika miaka ya hivi karibuni uhusiano wa Marekani na China umekumbwa na misukosuko mingi, na vita vya kibiashara na malumbano makali yameshika kasi zaidi baina ya nchi hizo mbili. Maambukizi ya virusi vya corona na taathira zake mbaya kwa upande mmoja, na uzembe na kufeli serikali ya Donald Trump katika mapambano dhidi ya virusi hivyo katika upande wa pili vimemfanya kiongozi huyo aanzishe vita vya maneno dhidi ya maafisa wa China na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kujinasua na lawama na ukosoaji mkubwa wa ndani na nje ya nchi. Katika kipindi hiki cha kukaribia uchaguzi wa rais wa Marekani, Trump ambaye anaandamwa na jinamizi kubwa la ukosoaji wa wataalamu na wanasiasa wa nchi hiyo, anafanya jitihada kubwa za kusafisha sura yake mbele ya Wamarekani. Kwa msingi huo anaituhumu China kwamba ilichelewa kutangaza janga na maambukizi ya corona na kutoa takwimu zisizo sahihi kuhusu maambukizi ya virusi hivyo.

Takwimu zinaonesha kuwa Wamarekani zaidi ya laki mbili wameaga dunia kutokana na virusi vya corona, na nchi hiyo ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu waliofariki dunia na vilevile idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa virusi hivyo. Uhaba wa vyombo vya tiba vinavyohitajika kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya corona, kushindwa kwa sehemu kubwa ya jamii ya Wamarekani kununua dawa na matibabu kutokana na gharama zake kubwa, siasa mbovu za Donald Trump kuhusiana na sheria za kipindi cha maambuizi ya corona na upungufu mkubwa wa zana zinatotumika kupima virusi hivyo (test kit), yote hayo na mengine yamezidisha kiwango cha maambukizi na idadi ya watu wanaoaga dunia kutokana na ugonjwa wa COVID-19 nchini Marekani.

Wamarekani zaidi ya laki mbili wameaga dunia kutokana na virusi vya corona

Suala hili, hasa katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani, linadhihirisha zaidi udhaifu mkubwa wa utendaji wa serikali ya Donald Trump. Kwa msingi huo kiongozi huyo anafanya jitihada kubwa za kujinasua katika kinamasi hicho kupitia njia ya kuanzisha vita vya kipropaganda dhidi ya China na Iran.

Dr Mike Ryan ambaye ni afisa wa ngazi za juu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) anasema: "WHO haina taarifa zozote zinazothibitisha madai ya Marekani dhidi ya China. Si hayo tu bali hata vyombo vya upelelezi na ujasusi vya Marekani vimetangaza kuwa, virusi vya corona havikutengenezwa na mwanadamu."

Ndani ya Marekani kwenyewe pia Donald Trump anayashinikiza mashirika mbalimbali yatangaze kupatikana kwa chanjo ya corona haraka iwezekanavyo ili aweze kutumia suala hilo kisiasa katika kampeni za uchaguzi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wachambuzi wa mambo wanasema ushindi wa Trump dhidi ya mgombea wa chama cha Democratic, Joe Biden, unategemea suala la kuwa na turufu kubwa kama vile kupatikana chanjo ya corona katika kipindi cha kabla ya uchaguzi huo.

Joe Biden na Trump

Kimebakia kipindi ca chini ya miezi miwili sasa hadi siku ya uchaguzi wa rais nchini Marekani na katika kipindi hiki Donald Trump amejikita zaidi katika masuala mawili muhimu. Kwanza ni kujaribu kutetea hatua yake ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambako kumekosolewa sana ndani ya Marekani na katika jamii ya kimataifa kutokana na kwamba kumekiuka sheria za kimataifa. Na pili ni kujaribu kuficha athari mbaya za kufeli kwa serikali yake katika kupamaba na kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Hata hivyo inaonekana kuwa, Wamarekani hawakubali janja na mbinu zinazotumiwa na Trump kupotosha sura halisi, na kura za maoni zinaonesha kuwa, uwezekano wa kupata ushindi Joe Biden ni mkubwa zaidi kuliko mpinzani wake huyo wa chama cha Republican.  

Tags

Maoni