Sep 25, 2020 02:33 UTC
  • Lavrov: Russia haikubaliani na takwa la Marekani la kukata ushirikiano na Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema nchi yake haikubaliani na takwa la Marekani la kuitaka ikate ushirikiano wake na Iran.

Sergey Lavrov ameyasema hayo katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari aliofanya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif huko mjini Moscow, mara baada ya mazungumzo ya pande mbili baina yao.

Amesema, Moscow na Tehran zimekusudia kustawisha mashirikiano yao ya kibiashara licha ya vikwazo vinavyowekwa na Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amebainisha kuwa, hatua za Marekani za kujaribu kufufua vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran havina muelekeo wowote. Lavrov ameongeza kuwa Russia na Iran zinapinga vikali pia hatua za Marekani za kujaribu kuweka vikwazo visivyo na mpaka vya silaha dhidi ya Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kwamba, Moscow inataka kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu pamoja na uwekezaji mitaji nchini Iran.

Kikao cha Baraza la Usalama la UN

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria kugonga mwamba Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na akasema: Takwa la Marekani la kurejeshwa maazimio yaliyopita dhidi ya Iran limekabiliwa na upinzani wa jamii ya kimataifa, na hilo ni pigo na kushindwa kukubwa kabisa kwa Marekani.

Mohammad Javad Zarif amesema, ana matumaini pia kuwa ifikapo Oktoba 20 wakati Russia itakaposhika urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, nchi hiyo itaendelea kulinda itibari na heshima ya baraza hilo kwa kukabiliana na harakati za Marekani za kuhalifu sheria.../

Tags

Maoni