Sep 25, 2020 02:34 UTC
  • Donald Trump
    Donald Trump

Rais wa Marekani ametabiri kuwa huenda hatima ya matokeo ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ikaamuliwa na Mahakama Kuu.

Donald Trump amesema, kwa maoni yake kuna uwezekano matokeo ya uchaguzi wa rais utakaofanyika tarehe 3 Novemba yakaamuliwa na Mahakama Kuu ya nchi hiyo.

Trump alitoa kauli hiyo jana Alkhamisi wakati siku ya Jumatano alipoulizwa kama atakabidhi madaraka kwa njia ya amani endapo atashindwa katika uchaguzi huo, alisema, atasubiri aone nini kitatokea kwa sababu kwa mtazamo wake yeye, masanduku ya kupigia kura hayana udhibiti.

Rais huyo wa Marekani alitoa matamshi hayo ukiwa ni mwendelezo wa upinzani wake dhidi ya utaratibu wa kupiga kura kwa njia ya posta ambao unaungwa mkono na Wademocrat na baadhi ya magavana wa majimbo ya nchi hiyo.

Wakati huohuo Trump ametetea uamuzi wake wa kuteua jaji wa kujaza nafasi ya Jaji Ruth Bader Ginsburg wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo aliyefariki.

Trump na mkewe Melania katika mazishi ya Jaji Ruth Bader Ginsburg

Ginsburg, ambaye ni mmoja wa majaji tisa wa Mahakama Kuu ya Marekani alifariki dunia siku ya Jumamosi iliyopita.

Mahakama Kuu ya Marekani ndicho chombo cha juu kabisa cha kutatua mizozo ndani ya nchi hiyo na ndiyo inayotoa uamuzi wa mwisho pia kuhusiana na tofauti zinazozuka kati ya serikali na bunge.

Seneta Ted Cruz wa chama cha Republican alisema hivi karibuni kuwa ikiwa Mahakama Kuu ya Serikali ya Federali haitakuwa na wajumbe tisa kuna hatari ya kushuhudiwa uchaguzi wenye mvutano mkubwa nchini humo.

Wakati tarehe ya uchaguzi wa rais wa Marekani inazidi kukaribia huku Trump akifanya juu chini ili asishindwe katika uchaguzi huo, hadi sasa maafisa kadhaa wa nchi hiyo wametahadharisha juu ya hatari na matokeo mabaya ya kutoshinda Trump katika kinyang'anyiro hicho.../

 

Tags

Maoni