Sep 25, 2020 02:34 UTC
  • Watafiti: China inasimamia kambi zaidi ya 380 za kuwekea watu kizuizini katika eneo la Xinjiang

Mtandao wa serikali ya China wa kambi za kuwekea watu kizuizini katika eneo la Xinjiang lililoko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ni mkubwa zaidi ya ilivyokuwa ikifikiriwa na ungali unaendelea kupanuliwa.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti mpya uliofanywa na Taasisi ya Sera za Kistratejia ya Australia (The Australian Strategic Policy Institute) ASPI.

Ripoti hiyo ya ASPI imeeleza kwamba, kuna vituo zaidi ya 380 vinavyoshukiwa kuwa ni kambi za kuwekea watu kizuizini katika eneo hilo, ambazo Umoja wa Mataifa unasema, katika miaka ya karibuni, zimekuwa zikitumiwa kuwashikilia watu zaidi ya milioni moja wa jamii ya Uighurs na wa jamii zinginezo, wengi wao wakiwa ni Waislamu wanaozungumza Kituruki.

Hayo yanaripotiwa wakati serikali ya Beijing inasema, inapunguza idadi ya kambi hizo zinazoelezwa kuwa zinatumika kwa ajili ya mpango wa utoaji mafunzo ya amali na "upigaji msasa" ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na tishio la fikra za kufurutu mpaka.

Waislamu wa jamii ya Uighurs wakikandamizwa na vikosi vya usalama vya serikali ya China

Taasisi ya Sera za Kistratejia ya Australia imesema, idadi ya vituo hivyo ni kubwa zaidi kwa asilimia 40 kuliko ilivyokuwa imekadiriwa hapo awali.

Watafiti wa ASPI wametumia picha za satalaiti, maelezo ya mashuhuda, ripoti za vyombo vya habari na nyaraka rasmi za zabuni za ujenzi ili kuweza kubaini vituo hivyo vya kuwekea watu kizuizini kutokana na kuta ndefu vilizozungushiwa, minara ya ulinzi na uzio uliowekwa ndani yake.

Hivi karibuni, serikali ya China ilitoa waraka wa kujisafisha kutetea sera zake katika eneo la Xinjiang, ikisisitiza kuwa programu za mafunzo, mipango ya kazi na elimu bora inayotoa huko vinamaanisha kuboreka kwa hali ya maisha ya watu wa eneo hilo.../

Tags

Maoni