Sep 25, 2020 07:33 UTC
  • Maseneta wa Marekani: Siasa za Trump zimeifanya Iran iwe imara zaidi

Maseneta wa chama cha Democratic nchini Marekani wamekiri kwamba siasa za serikali ya Washington zimepelekea kuimarika zaidi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutengwa Marekani duniani.

Kituo cha habari cha Al-Monitor cha Washington DC kimeripoti kuwa, kikao cha jana Alkhamisi cha Kamati ya Uhusiano wa Kigeni cha Baraza la Seneti la Marekani kilichohudhuriwa na Mjumbe Maalumu wa Rais Donald Trump katika Masuala ya Iran, Eliot Abrams, kimekosoa vikali siasa za ikulu ya rais wa nchi hiyo, White House mkabala wa Iran. 

Seneta Bob Menendez mjumbe wa Kamati ya Uhusiano wa Kigeni ya Baraza la Seneti ya Marekani ambaye pia alihudhuria kikao hicho ameashiria matamshi yaliyotolewa na kamanda wa jeshi la kigaidi la Marekani CENTCOM, Kenneth F. McKenzie kuhusu ongezeko la mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na kukanusha madai ya White House inayosema kuwa Iran imetengwa na kudhoofika.

Seneta Bob Menendez

Seneta Chris Murphy pia ameashiria uhusiano wa Iran na serikali ya Syria na madai kwamba Iran inaisaidia harakati ya Ansarullah huko Yemen na kusema: Kwa sasa Iran imekuwa imara na yenye nguvu zaidi katika kanda ya magharibi mwa Asia ikilinganisha na mwishoni kwa kipindi cha utawala wa Barack Obama. 

Kwa upande wake seneta Ben Cardin wa Maryland amezungumzia uhusiano unaoyumbayumba wa Marekani na washirika wake wa Ulaya kuhusiana na kadhia ya Iran na kusema kuwa, serikali ya Trump ilitengwa na nchi za Ulaya baada ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. 

Itakumbuka kuwa mwezi uliopita wa Agosti wanachama wote wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, isipokuwa nchi ndogo ya Jamhuri ya Dominican, walipinga muswada wa Marekani wa kutaka kuhuishwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran. Hatua hiyo iliashiria jinsi Marekani inavyoendelea kutengwa hata baina ya washirika wake wa Ulaya.  

Tags

Maoni