Sep 25, 2020 12:54 UTC
  • Shaka na atiati ya kukabidhiwa madaraka kwa amani baada ya uchaguzi wa urais wa Marekani

Ukiwa umesalia mwezi mmoja na ushee kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais wa Marekani, kila siku zinavyosonga mbele ndivyo jamii ya nchi hiyo inavyozidi kushuhudia kauli za mabishano na malumbano zenye kuzusha taharuki zinazotolewa kuhusiana na uchaguzi huo.

Kauli mpya iliyotolewa hivi karibuni ni ya rais Donald Trump ambaye amesisitiza kwa mara nyingine kuwa udanganyifu mkubwa utafanywa katika uchaguzi wa urais; na akatabiri kwamba matokeo ya uchaguzi huo yataamuliwa na mahakama kuu ya serikali ya shirikisho. Na kwa sababu hiyo pia Trump amesema, lazima ateuliwe jaji wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha jaji wa mahakama kuu ya shirikisho Ruth Bader Ginsburg kabla ya kufanyika uchaguzi. Na kwa mara nyingine tena pia rais huyo wa Marekani amekataa kutoa tamko na hadi ya wazi kwamba atakabidhi madaraka kwa salama na amani baada ya uchaguzi wa urais wa Novemba 3 endapo atashindwa katika uchaguzi huo.

Kuna hofu ya kuzuka machafuko endapo Trump atashindwa katika uchaguzi

Matamshi hayo ya Trump yamekuwa na umuhimu zaidi ikizingatiwa kuwa chunguzi za maoni zimkeuwa zikionyesha kwamba Joe Biden, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democrat anaendelea kupewa nafasi kubwa zaidi ya kumbwaga Trump katika kinyang'anyiro hicho. Hiyo ni baada ya kutangazwa kuwa, kuna uwezekano wa mgombea huyo wa Wademocrat kupata kura nyingi zaidi hata katika baadhi ya majimbo ambayo kwa miaka na miaka, yamekuwa ni ngome ya chama cha Republican yakiwemo ya Georgia na Texas. Inaelezwa kwamba, hali si shwari pia kwa chama cha Republican katika aghalabu ya majimbo ambayo yalimwezesha Trump kumshinda Hillary Clinton, mpinzani wake wa chama cha Democrat katika uchaguzi mkuu wa 2016.

Kutokana na hali hiyo, inatarajiwa kuwa Trump na waungaji mkono wake watayapinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo na maeneo mengi ya upigaji kura na kuwasilisha malalamiko mahakamani. Bila shaka kuwasilishwa malalamiko mahakamani ya kupinga mchakato wa uendeshaji uchaguzi na utaratibu wa kuhesabu kura ni jambo lenye historia ndefu nchini Marekani. Itakumbukwa kuwa, mwaka 2000 malalamiko yaliyoibuliwa katika jimbo la Florida yaliishia kwenye mahakama kuu ya shirikisho; na hatimaye kwa kutumia turufu ya uwepo wa idadi kubwa zaidi ya majaji wahafidhina kulinganisha na waliberali, mahakama hiyo ikatoa uamuzi wa kusitisha zoezi la kuhesabiwa tena kura huko Florida na hivyo kumwezesha George W. Bush wa chama cha Republican kutangazwa mshindi dhidi ya mpinzani wake Al Gore wa chama cha Democrat.

Al Gore (kushoto) na Bush katika mdahalo wa uchaguzi wa urais wa 2000

Kwa muda mrefu sasa, Trump pia amekuwa akitangaza kwamba hatoshindwa katika uchaguzi wa Novemba isipokuwa, kwa anavyodai mwenyewe, kama Wademocrat watautumia upigaji kura kwa njia ya posta kufanya udanganyifu na uchakachuaji mkubwa. Lakini katika upande wa pili pia Kamala Harris, mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya chama cha Democrat  amesema, Wademocrat watashindwa tena mara hii ikiwa tu Russia itaingilia tena uchaguzi wa Marekani.

Kwa maneno mengine ni kwamba, kinyume na ilivyokuwa katika duru zilizopita, si Warepublican wala  Wademocrat watakaokubali matokeo ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka huu pasi na kuwasilisha malalamiko katika vyombo vya mahakama. Pamoja na hayo, suali muhimu zaidi la kujiuliza ni, je rais wa Marekani atakubali matokeo endapo atashindwa katika uchaguzi, na je atakuwa tayari kukabidhi madaraka kwa njia za amani kwa rais mpya atakayechaguliwa au la?

Kusema kweli Trump hajatoa jibu la wazi hadi sasa kila alipoulizwa suali hilo mara kadhaa na waandishi wa habari, bali kila mara amekuwa akisema "itabidi tuone nini kitatokea". Matamshi hayo yamezusha wasiwasi hata ndani ya chama chake cha Republican.

Joe Biden (kushoto) na Trump

Seneta Mitt Romney, ambaye aligombea na kushindwa katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2012 ni miongoni mwa wanachama waandamizi wa Republican ambao wameyakosoa majibu hayo tata yanayotolewa na Trump. Romney ameandika katika ukurasa wa Twitter: "Msingi wa demokrasia ni kukabidhi madaraka kwa njia ya amani...wazo lolote la kuonyesha kwamba kuna uwezekano wa rais kutoheshimu hakikisho hili la kikatiba, halitasawariki na wala halikubaliki."

Pamoja na yote hayo, katika miaka ya karibuni Donald Trump ameonyesha mara kadhaa kuwa hajali wala habali kuchukua hatua ambazo hazitasawariki wala hazikubaliki.../ 

 

Maoni