Sep 26, 2020 05:55 UTC
  • Sisitizo la maseneta wa Marekani, vikwazo vya Trump kwa Iran vimeshindwa

Serikali ya Donald Trump nchini Marekani na hatua yake ya kujitoa kijeuri katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA hapo mwezi Mei 2018 kama sehemu ya siasa zake za kuiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha ambavyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuwekewa mfano wake katika historia yake yote, imezidi kufeli kiasi kwamba sasa maseneta wa chama cha Democrats wanamshutumu na kumlaumu vikali Trump kwa siasa zake mbovu.

Katika kikao cha Kamati ya Uhusiano wa Nje ya Baraza la Sanate la Marekani kilichofanyika Alkhamisi tarehe 24 Septemba 2020, na kuhudhuriwa na Elliott Abrams, mwakakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran, maseneta wa chama cha Democrats walimlaumu vikali Donald Trump kwa siasa zake mbovu mbele ya Tehran na kusisitiza kuwa vikwazo vyake vya kiwango cha juu dhidi ya Iran vimefeli. Wamesema, si tu vikwazo hivyo vimeifanya Iran ijiimarishe zaidi, lakini pia Tehran imezidi kujiwekea kinga za kukabiliana na hali ngumu inazokabiliana nazo. Seneta Bob Menendez ambaye ni mjumbe mwandamizi katika Kamati ya Uhusiano wa Nje ya Baraza la Sanate la Marekani amegusia jinsi mashambulio dhidi ya wanajeshi wa Marekani yalivyoongezeka sana huko Iraq na kuongeza kuwa, Trump na serikali yake wanasema uongo wanapodai kuwa Iran imetengwa na imedhooofika. Seneta Chris Murphy yeye amesema, uhusiano wa Iran na Syria umezidi kuwa imara, pia amedai kusaidiwa na Iran harakati ya Answarullah ya Yemen na kusema, mambo hayo yanaonesha kwamba Iran imezidi kuwa na nguvu ikilinganishwa na hali yake mwishoni mwa urais wa Barack Obama. Naye Seneta Ben Cardin amezungumzia jinsi Trump na serikali yake walivyovuruga vibaya uhusiano wa Marekani na waitifaki wake wa jadi wa barani Ulaya kutokana na suala hilo hilo la Iran na kusisitiza kuwa, kitendo cha Trump cha kujitoa katika mapatano ya JCPOA kimezifanya nchi za Ulaya zijiweke mbali na Marekani. 

Brian Hoo mwenye chuki kubwa na taifa la Iran ambaye amelazimika kujiuzulu baada ya kushindwa siasa zake

 

Kufeli siasa za Trump mbele ya Iran hakuzungumziwi na wapinzani wa Trump ndani ya Marekani na washirika wa nje wa Marekani tu, bali mara chungu nzima viongozi wa sekta mbalimbali na wachambuzi wa mambo ndani na nje ya Marekani wamekuwa wakikariri kwamba siasa za Trump zimefeli mbele ya Iran. Paul Pillar, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Marekani anasema: Kuna ishara nyingi zinazowafanya wataalamu na wachambuzi wa mambo waamini kwamba siasa za Marekani za kuweka vikwazo vikubwa ili kuifanya Iran isalimu amri, zimefeli. Moja ya ishara hizo ni pale tunapoona hata wale waliokuwa wakiunga mkono siasa hizo, nao wanakiri kushindwa kwake

Kusema kweli, tofauti na madai ya mara kwa mara ya rais wa Marekani, Donald Trump na baadhi vya viongozi wa ngazi za juu wa serikali yake hasa waziri wake wa mambo ya nje, Mike Pompeo, uhakika ni kuwa siasa hizo za Marekani zimefeli kufikia lengo lake lolote kutokana na taifa la Iran kukabiliana na vikwazo hivyo vya kiwango cha juu vya Marekani kwa kutumia "muqawama wa kiwango cha juu." Miradi ya nyuklia ya Iran ambayo kimsingi ni ya amani kikamilifu inaendelea kama kawaida bali kwa ufanisi zaidi, siasa za Iran katika eneo hili hazijabadilika na katika upande wa kiulinzi pia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezidi kuwa imara hususan katika upande wa nguvu zake za makombora.  

Baraza la Senate la Marekani

 

Ijapokuwa Washington inadai kuwa, vikwazo vyake vya kiwango cha juu ambavyo havijawahi kuwekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika historia yake yote, vitailazimisha Tehran ikubali masharti 12 yaliyotangazwa na Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani mwezi Mei 2018, lakini ukweli ni kuwa, muqawama wa kupigiwa mfano wa taifa la Iran mbele ya vikwazo hivyo umeivunja moyo na kuikatisha tamaa serikali ya Trump kiasi kwamba viongozi mbalimbali wa serikali yake wamejiuzulu au kufutwa kazi. Kiongozi wa karibuni kabisa ni Brian Hook, aliyekuwa mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran ambaye alichukua misimamo ya kiuadui mno dhidi ya taifa la Iran, lakini hatimaye ameshindwa na kujiuzulu.

Tags

Maoni