Sep 26, 2020 12:36 UTC
  • Imran Khan
    Imran Khan

Waziri Mkuu wa Pakistan amesema serikali ya Kihindu ya India inaunga mkono na kuchochea chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.

Imran Khan alisema hayo jana Ijumaa katika hotuba aliyoitoa katika mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea kufanyika kwa njia ya intaneti kupitia mawasiliano ya video, ambapo pia ameikosoa serikali ya New Delhi kwa kuchukua hatua za kuimarisha udhibiti wake katika eneo lenye Waislamu wengi la Kashmir.

Amesema harakati za chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) zimekita mizizi nchini India na kuhatarisha maisha ya Waislamu zaidi ya milioni 200 wa nchi hiyo ya Asia.

Khan amesema: "Nasikitika kusema kuwa, hii leo nchi moja duniani ambayo dola linafadhili chuki dhidi ya Uislamu ni India. Haya yote yametokana na idiolojia (potofu) ya RSS inayotawala (India). Wanaitakidi kuwa India ni mahususi kwa Wahindu pekee, na raia wengine hawana haki."

Jinai za Wahindu na maafisa usalama wa India dhidi ya Waislamu wa Kashmir

Waziri Mkuu wa Pakistan amesema amani ya kudumu na uthabiti havitashudiwa Kusini mwa Asia hadi pale mgogoro kuhusu maeneo ya Kashmir na Jammu utakapopatiwa ufumbuzi kwa kutegemea misingi ya sheria za kimataifa. Mwezi Agosti mwaka jana, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi alibatilisha mamlaka ya kujitawala eneo la Kashmir hatua ambayo Pakistan iliitaja kuwa kinyume cha sheria.

Imran Khan ameitaka jamii ya kimataifa ichunguze ugaidi wa kiserikali na jinai za kutisha na zinazokanyaga haki za binadamu zilizofanywa na raia na maafisa usalama wa India dhidi ya Waislamu wa maeneo ya Jammu na Kashmir katika maandamano ya kulaani sheria hiyo tata.

Tags

Maoni