Sep 27, 2020 11:05 UTC
  • Malalamiko ya Marekani kwa UN, njama za kujaribu Washington kuficha kufeli kwake

Kufeli vibaya Marekani katika masuala mengi ya kimataifa yakiwemo ya kukabiliana na kirusi cha corona na njama zake za kutaka kurejesha vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran vikiwemo vya silaha kumewatia hamaki viongozi wa nchi hiyo na sasa kama kawaida ya Trump na serikali yake, wanaulaumu Umoja wa Mataifa wakidai haufanyi kazi zake ipasavyo.

Kelly Craft, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ameutuhumu umoja huo kuwa umeshindwa kutekeleza majukumu yake ya kuifanya dunia kuwa na amani zaidi na yenye demokrasia zaidi. Vile vile amekiri kuweko misimamo hasi ya nchi za dunia kuhusu Marekani na kudai kuwa hilo linatokana na chuki za nchi hizo kwa nchi yake. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa vile vile amedai kuwa, Umoja wa Mataifa unapaswa kuishukuru nchi yake kutokana na siasa zake zikiwemo za kuifanyia uadui Iran na eti kukusanya fedha nyingi za kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.

Ukweli wa mambo ni kwamba, serikali ya Trump inalaumiwa sana na nchi mbalimbali duniani kutokana na misimamo yake ya kujikumbizia kila kitu upande wake katika masuala na migogoro ya kimtaifa, suala ambalo linakwenda kinyume na maslahi ya kimataifa. Lawama hizo zinazotokana na maamuzi mengi hasi ya Washington, zinatoka kwa wapinzani na marafiki wa Marekani. Mfano wa wazi ni maamuzi hasi ya Marekani kuhusu Shirika la Afya Duniani WHO, kujitoa kwake kwenye shirika hilo na kulikatia misaada ya kifedha kwa madai kuwa WHO inashirikiana na China dhidi ya Marekani na vile vile kushindwa serikali ya Trump kukabiliana na kirusi cha corona na ugonjwa wa COVID-19.

Kelly Craf, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa

 

Kelly Craft amedai kuwa, Shirika la Afya Duniani halijafanya chochote cha maana zaidi ya kuwa msemaji wa serikali ya China. Donald Trump amefeli vibaya sana katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 kiasi kwamba, sasa hivi, karibu Wamarekani laki mbili na 10,000 wameshafariki dunia kutokana na ugonjwa huo na zaidi ya milioni saba na laki mbili na 88 elfu  wamekumbwa na ugonjwa huo hatari. Sasa Trump ambaye anachukia sana kulaumiwa, kama kawaida yake, hivi sasa pia amewatupia wengine lawama za kufeli kwake kukabiliana na ugonjwa huo. 

Ripota wa USA Today, Deirdre Shesgreen anasema, Trump na washauri wake wanalilaumu Shirika la Afya Duniani kuwa linashirikiana na China wakidai kuwa wakuu wa shirika hilo wameshindwa kuishawishi Beijing kuwa muwazi katika suala la kirusi cha corona.

Jambo jingine lililogusiwa na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ni kutengwa vibaya sana Washington katika Baraza la Usalama la umoja huo kuhusu kadhia ya kuirejeshea Iran vikwazo vya kimataifa kwa madai chapwa ya serikali ya Trump kwamba eti Iran haikuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Rais wa Marekani, Donald Trump

 

Ukweli ni kwamba, si Baraza la usalama tu lililopinga vikali madai hayo ya uongo ya Marekani, bali kiongozi wa ngazi za juu zaidi wa Umoja wa Mataifa yaani katibu Mkuu wa umoja wa huo António Guterrez naye pia ametangaza waziwazi kuwa hawezi kuchukua hatua yoyote kuhusu madai hayo ya Marekani ya kutaka kuirejeshea Iran vikwazo vya kimataifa vilivyoondolewa baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, kwani Washington imeshindwa kutoa ushahidi wa kuweza kuyakinaisha mataifa ya dunia kuhusu suala hilo.

Msimamo imara ambao haujawahi kutokea mfano wake ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia msimamo thabiti wa Guterrez umewahamakisha vibaya viongozi wa Marekani ambao wamejifanya kurejesha vikwazo hivyo dhidi ya Iran bila ya hata kupasishwa na Umoja wa Mataifa na kutishia kumuwekea vikwazo yeyote atakayeshindwa kuheshimu amri zake, majigambo ambayo nayo yamefeli baada ya kupingwa vikali na mataifa ya dunia. Lawama zilizotolewa hivi sasa na Marekani kwa Umoja wa Mataifa nazo zinaonesha hamaki kubwa zilizowachemsha viongozi wa Washington baada ya Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama kukataa kufuata siasa na matakwa yasiyoingia akilini na yaliyo kinyume cha sheria ya Marekani.

Maoni