Sep 27, 2020 13:41 UTC
  • Serikali ya Afghanistan: Taliban inatumia mbinu ya kupoteza muda katika mazungumzo

Mjumbe wa timu ya wawakilishi wa serikali ya Afghanistan katika mazungumzo ya amani ya Doha amelituhumu kundi la Taliban kuwa linatumia mbinu ya kupoteza muda katika mazungumzo hayo.

Nader Naderi amesema, kundi la Taliban linaweka vizingiti na kutoa visingizio ili kukwamisha kufikiwa makubaliano katika mazungumzo ya amani ya Doha.

Kwa mujibu wa mjumbe huyo wa timu ya wawakilishi wa serikali ya Kabul katika mazungumzo ya kutafuta suluhu na amani Afghanistan yanayofanyika katika mji mkuu wa Qatar, Taliban inataka yafanyike mazungumzo mengine mapya kuhusiana na baadhi ya vipengele vya makubaliano ya Februari 29 iliyofikia na Marekani mjini Doha.

Naderi amesema, kundi la Taliban linavishambulia vikosi vya usalama vya serikali pamoja na raia wa kawaida ili kuiweka kwenye mashinikizo serikali ya Kabul.

Wanamgambo wa kundi la Taliban

Ijapokuwa wawakilishi wa kundi la Taliban wako kwenye mazungumzo na ujumbe wa serikali, ya kusaka suluhu na kurejesha amani nchini Afghanistan lakini hujuma na mashambulio ya kundi hilo dhidi ya vikosi vya jeshi la serikali ya Kabul na hata raia wa kawaida wa Afghanistan yameshtadi; na watu wengi wameuawa na kujeruhiwa katika mashambulio yaliyofanywa hivi karibuni na kundi hilo.

Kauli zilizotolewa hivi kribuni na wawakilishi wa serikali ya Afghanistan huko Doha zinaashiria matumaini waliyonayo ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita katika duru ya sasa ya mazungumzo hayo, wakati kundi la Taliban linasisitiza kuwa ni muhali kupatikana haraka mwafaka wa kusitisha mapigano baina ya pande mbili.../

 

Tags

Maoni