Sep 27, 2020 13:58 UTC
  • Wanajeshi wa India na Pakistan wafyatuliana tena risasi kwenye mpaka wa eneo la Kashmir

Askari mmoja wa Pakistan ameuawa katika mapigano mapya ya mpakani yaliyozuka katika eneo la Kashmir kati ya wanajeshi wa nchi hiyo na India.

Jeshi la Pakistan limeeleza katika taarifa kwamba, askari wa mpakani wa India usiku wa kuamkia leo walikiuka mkataba wa kusitisha vita kwa kushambulia maeneo ya mpakani ya Kot Katira yaliyoko kwenye eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, askari mmoja wa jeshi la Pakistan aliuawa katika shambulio hilo.

Taarifa ya jeshi la Pakistan imeongeza kuwa, vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimetoa jibu kali kwa hatua hiyo ya jeshi la India na kuvisababishia hasara kubwa vituo vya mpakani vya jeshi hilo.

Siku ya Alkhamisi iliyopita Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan iliwaita maafisa waandamizi wa ubalozi wa India mjini Islamabad kulalamikia ukiukaji mkataba wa usitishaji vita katika maeneo ya mpakani unaofanywa na vikosi vya New Delhi ambao ulisainiwa na pande mbili mwaka 2003.

Pakistan inasema: Kwa miaka na miaka, India imeweka maelfu ya askari wa jeshi lake katika maeneo ya Kashmir iliyo chini ya udhibiti wake; na katika kipindi cha miongo mitatu ya karibuni imeua maelfu ya watu katika eneo hilo.

Wananchi Waislamu wa Kashmir wanataka kutekelezwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalohusiana na uitishaji kura ya maamuzi ya kuainisha hatima ya eneo hilo, lakini serikali ya India inapinga utekelezwaji wa azimio hilo.../

Tags

Maoni