Sep 28, 2020 07:52 UTC
  • Mgogoro waongezeka Marekani, wagonjwa wa corona wapindukia milioni 7 na laki 3

Idadi ya wagonjwa wa corona waliothibitishwa nchini Marekani imevunja tena rekodi. Sasa imepindukia watu milioni saba na laki tatu.

Chuo Kikuu cha Johns Hopkins cha Marekani, usiku wa kuamkia leo kimetangaza kuwa, wagonjwa 36 elfu na 196 wa COVID-19 wamethibitishwa nchini Marekani katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia wakati wa kutangazwa habari hiyo na hivyo kuifanya Marekani kuvunja tena rekodi ya idadi kubwa kupindukia ya wagonjwa wa corona.

Huku hayo yakiripotiwa, mtandao wa taarifa za COVID-19 unaojulikana kwa jina la Worldmeters umeripoti kuwa, idadi ya wagonjwa wa corona nchini Marekani hadi kufikia leo asubuhi ilikuwa ni zaidi ya milioni 7 na laki tatu 3 na 21,343, huku idadi ya Wamarekani waliopoteza maisha kulingana na takwimu za serikali ya nchi hiyo wakipindukia laki mbili na 9,453. 

Marekani inaongoza kwa mbali sana duniani kwa idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vya COVID-19

 

Marekani inaongoza kwa mbali sana kwa idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na ugonjwa hatari wa COVID-19 huku rais wa nchi hiyo Donald Trump akizidi kushutumiwa kwa kufanya uzembe na kusababisha balaa kubwa kwa wananchi wa Marekani.

Serikali ya Marekani ilichelewa sana kuanza kuchukua vipimo vya wagonjwa wa corona. Wakati huo Trump alikuwa anaifanyia istihzai China kutokana na kukumbwa na ugonjwa huo. Sasa hivi Marekani ina upungufu mkubwa wa vifaa vya kupimia na kupambana na ugonjwa huo.

Nchi zinazofuatia kwa wagonjwa wengi wa corona baada ya Marekani ni India, Brazil, Russia, Colombia, Peru na Uhispania. Hadi kufikia leo asubuhi, watu 33,310,953 walikuwa wamekumbwa na corona kote duniani. Kati ya hao, 24,639,064 walikuwa wameshapata afueni na 1,002,452 walikuwa wameshafariki dunia.

Tags

Maoni