Sep 30, 2020 02:41 UTC
  • Kuwasili shehena mpya ya nishati ya mafuta ya Iran nchini Venezuela

Licha ya vizingiti, ukwamishaji mambo na mashinikizo ya Marekani, shehena ya pili ya nishati ya mafuta ya Iran imewasili nchini Venezuela.

Kuwasili katika maji ya Venezuela meli ya mafuta ya Forest kutoka Iran, kumepigwa hatua kubwa na madhubuti katika ustawi wa uhusiano wa Iran na Venezuela. Meli ya Mafuta ya Forest, ni meli ya kwanza kati ya meli tatu za mafuta ya Iran ambazo zilianza safari ya kuelekea Venezuela kwa mara ya pili. Meli nyingine mbili nazo karibuni hivi zinatarajiwa kuwasili katika maji ya nchi hiyo.

Kwa muda sasa Venezuela imekuwa chini ya mashinikizo makubwa ya Marekani ambapo katika miezi ya hivi karibuni nchi hiyo ya Latini Amerika imekabiliwa na uhaba mkubwa wa nishati ya mafuta. Kuchakaa kwa vituo vya kusafishia mafuta sanjari na vikwazo vya Marekani ni mambo yaliyopelekea utunzaji na ukarabati wa vituo hivyo usiwezekane na kuifanya nchi hiyo ikabiliwe na tatizo la kushindwa kujidhaminia nishati ya mafuta. Ukweli wa mambo ni kuwa, vikwazo vya Marekani vimeifanya kazi ya ukarabati na utunzaji wa vituo hivyo vya kusafishia mafuta kukabiliwa na kibarua kigumu.

Katika miezi ya hivi karibuni uhaba wa mafuta nchini Venezuela ulishadidi zaidi kutokana na Shirika la Mafuta la Rosneft kusitisha shughuli zake tangu Machi mwaka huu kutokana na na mashinikizo na vikwazo vya Marekani. Mwaka uliopita, shirika hilo la Rosneft liligeuka na kuwa kiunganishi kikuu cha uuzaji mafuta na udhamini wa nishati hiyo kwa Venezuela. Hata hivyo, Marekani ilianza kuyalenga kwa vikwazo mashirika yaliyoko chini ya shirika hilo la Russia kwa kisingizio kwamba, yanasaidia biashara ya mafuta ya Venezuela.

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela

 

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, vikwazo vya Wizara ya Hazina ya Marekani katika miaka mitatu ya hivi karibuni, vimekuwa na mchango na nafasi muhimu ya kutoa pigo dhidi ya shughuli za Shirika la Taifa la Mafuta la Venezuela na kupungua kiwango cha uzalishaji na usambazaji wa nishati hiyo.

Licha ya vitisho vya Marekani, lakini taifa la Iran likiwa mshirika muhimu wa Venezuela, huko nyuma pia imewahi kutuma nchini humo meli 5 zilizokuwa zimesheheni nishati ya mafuta na hivyo kusaidia pakubwa kuziba pengo la uhaba wa nishati hiyo katika nchi hiyo ya Amerika ya Ltini. Hatua hii ya Iran ilikabiliwa na vitisho na misimamo mikali ya viongozi wa Washington. Viongozi wa Marekani walitishia kwamba, wangezikamata na kuzishikilia meli za mafuta za Iran. Hata hivyo licha ya vitisho hivyo, lakini meli hizo za mafuta ziliwasili salama salimini katika maji ya Venezuela; hatua ambayo inathminiwa na wajuzi wa mambo kuwa, ni pigo kubwa kwa siasa za kibabe za Marekani.

Abdul-Bari Atwan mtaalamu wa masuala ya kisiasa na mwandishi nguli wa Kiarabu ameandika kuhusiana na kutumwa meli za mafuta za Iran nchini Venezuela kwamba: Kuwasili meli za mafuta za Iran katika fukwe za Venezuela ni sawa na kumzaba kibao Rais Donald Trump pamoja na ubeberu wa Marekani.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, Rais wa Marekani ameshindwa kuzuia himaya na uungaji mkono wa Iran kwa taifa la Venezuela pamoja na Nicolas Maduro Rais shujaa na aliyechaguliwa kihalali.  Hatua hii ya Iran imevunjia mbali mzingiro wa Marekani dhidi ya Venezuela.

Licha ya mashinikizo yote ya Marekani, lakini ushirikiano baina ya Iran na Venezuela umeimarika zaidi katika miezi ya hivi karibuni na mataifa haya mawili sasa yamo mbioni kunufaika na uwezo wa kila mmoja kwa ajili ya kuyashinda matatizo inayokabiliwa nayo. Kama alivyosisitiza Rais Nicolas Mafuro katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: Iran na Venezuela zina haki ya kujiainisha hatima na mustakabali wao, kujidhaminia amani na utulivu pia.

Kabla ya hapo pia, Rais Maduro alikuwa ametoa shukurani zake kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na himaya na uungaji mkono wake kwa serikali na wananchi wa nchi hiyo na kusisitiza kwamba, Venezuela haiko peke yake bali ina marafiki mashujaa ambao wamesimama pamoja nayo. Kufunguliwa duka la kwanza kubwa la bidhaa za Iran katika mji mkuu Caracas na wakati huo huo kuendelea ushirikiano wa Venezuela na Iran, kumeifanya serikali ya Trump iendelee kubwabwaja na kutoa vitisho hivi na vile.

Kuwasili meli ya mafuta ya Iran nchini Venezuela

 

Kama walivyosea wahenga kwamba, mfa maji haishi kutapatapa, viongozi wa Marekani wametangaza kuwa, wamo mbioni kuandaa mpango kabambe wa kuziwekea vikwazo takribani meli 50 za mafuta kwa shabaha ya kukata ushirikiano wa kibishara wa Iran na Venezuela.

Alaa kullihaal, kuwasili nchini Venezuela meli nyingine iliyobeba mafuta ya Iran, tena hii ikiwa na safari ya pili kwa meli hiyo, ni ishara ya wazi ya uwezo wa Iran na azma ya nchi mbili hizo ya kushirikiana kwa minajili ya kukabiliana na vitisho na vikwazo vya serikali ya Washington. Inaonekana kuwa, siyo Iran na Venezuela tu, bali akthari ya mataifa ya dunia yameshang’amua hila na hadaa za Marekani, hivyo hayako tayari tena kuwa vigaragosi wa Washington katika kutekeleza vitisho na siasa za vikwazo za dola hilo la kibeberu.

Tags

Maoni