Oct 14, 2020 16:14 UTC
  • Kuanza tena mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Afghanistan na Taliban nchini Qatar

Wawakilishi wa serikali ya Afghanistan na wa kundi la Taliban wameanza tena mazungumzo yao nchini Qatar ya kutafuta suluhu na kurejesha amani nchini Afghanistan. Pande hizo mbili zinakutana mara hii kujadili tofauti zilizopo baina yao ili kuweza kufikia mwafaka.

Msemaji wa ujumbe wa serikali ya Afghanistan katika mazungumzo hayo ya kutafuta amani Ahmad Nader Naderi amesema pande mbili za serikali na kundi la Taliban zimekubaliana kuendelea na mazungumzo ili kutatua masuala zinayohitilafiana.

Kutokana na hatua hiyo, ndiyo kusema kwamba, mazungumzo baina ya serikali ya Afghanistan na Taliban yameanza tena baada ya kusita kwa muda wa siku 12.

Makamu wa Rais wa Afghanistan Sarvar Danesh alisema hivi karibuni kuwa, serikali ya Kabul imependekeza kwa Taliban kwamba, Qur'ani, Sunna na sharia za Kiislamu viwe ndiyo marejeo na msingi wa kutatulia tofauti zao; lakini kundi la Taliban lingali linang'ang'ania kutumiwa mkataba wa makubaliano yaliyofikiwa baina yake na Marekani na fiqhi ya madhehebu ya Hanafi kama marejeo ya kutumiwa kutatulia tofauti hizo.

Rais Ashraf Ghani (kulia) na Mkuu wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa Abdullah Abdullah

Wakati huohuo Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan na Mkuu wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la nchi hiyo Abdullah Abdullah wamekutana kujadili mwenendo wa mazungumzo ya amani yanayoendelea kati ya serikali ya nchi hiyo na Taliban.

Makubaliano waliyofikia wawakilishi wa serikali ya Afghanistan na wa kundi la Taliban ya kurudi tena kwenye meza ya mazungumzo ya kutafuta amani ambayo yanafanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha yanaweza kuwa ni ishara ya pande hizo mbili kubaini ulazima wa kulegeza misimamo yao ili kuweza kukomesha vita na kurejesha uthabiti na utulivu nchini Afghanistan.

Ijapokuwa Taliban imekuwa ikidai kila mara kwamba iko tayari wakati wowote ule kuendelea kupigana vita nchini Afghanistan lakini ukweli ni kwamba baada ya kupita karibu miongo miwili ya vita nchini humo kundi hilo linaendelea kudhoofika; na uamuzi wake wa kukubali kufanya mazungumzo unaashiria hamu liliyonayo ya kuhitimisha vita na mapigano nchini Afghanistan.

Pamoja na hayo, sambamba na kuendelea mazungumzo baina ya Waafghanistani nchini Qatar, kundi la Taliban limeshadidisha hujuma na mashambulizi yake ndani ya Afghanistan kwa shabaha ya kuishinikiza serikali ya Kabul pamoja na wawakilishi wake katika mazungumzo ya amani ya mjini Doha.

Mazungumzo ya Doha ya amani ya Afghanistan yakiwa yanaendelea

Ripoti za karibuni kabisa kutoka Afghanistan zinaeleza kuwa, Taliban imeanzisha hujuma na mashambulio makubwa katika mkoa wa Helmand; na kwa mujibu wa baadhi ya duru, sehemu kadhaa za miji ya Lashgar Gah, Nad-ali na Naveh zimetekwa na kudhibitiwa na wapiganaji wa kundi hilo.

Hata kama kulikuweko na matumanini kwamba kundi la Taliban litapunguza mashambulizi yake ndani ya Afghanistan sambamba na kufanyika mazungumzo ya amani ya nchi hiyo mjini Doha, lakini lilichofanya kundi hilo ni kushadidisha hujuma na mashambulio ili kuweza kuishinikiza serikali ya Afghanistan izidi kulegeza msimamo na kukidhi matakwa mengi zaidi ya Taliban.

Kwa sasa, kisingizio kikubwa zaidi kinachotumiwa na Taliban ili kutatiza na kukwamisha mchakato wa mazungumzo ya amani na serikali ya Afghanistan ni kuhalifu Marekani kutekeleza ahadi na makubaliano iliyofikia na kundi hilo kuhusiana na Afghanistan; na ukweli ni kwamba kitendo cha serikali ya Washington cha kuhalifu ahadi zake kimeathiri na kuvuruga mazungumzo baina ya Waafghanistani yaliyoanza tena hivi sasa.

Marekani na Taliban zikisaini mkataba wa makubaliano Doha

Taliban imetoa sharti kwamba makubaliano kamili kati yake na serikali ya Afghanistan katika mazungumzo ya Qatar yatafikiwa kwa kuondoka majeshi yote ya kigeni katika ardhi ya Afghanistan; na kutotekeleza Marekani ahadi ilizotoa kuhusiana na suala hilo kumeyaelekeza mazungumzo hayo kwenye mkondo wa kufeli.

Tukizingatia kinachoendelea katika mwenendo wa mazungumzo baina ya Waafghanistani huko nchini Qatar, tuna kila sababu ya kusema kuwa, serikali ya Marekani ndiye msababishaji mkuu wa kufeli mazungumzo hayo kwa sababu kuhalifu kwake ahadi iliyotoa ya kuondoa majeshi yake Afghanistan kunahatarisha fursa iliyopatikana ya kuhitimisha mapigano na machafuko nchini humo.

Hivi sasa kuna wasiwasi kuwa, hata kama yatafikiwa makubaliano kati ya serikali ya Afghanistan na Taliban katika mazungumzo ya amani ya Doha, ung'ang'anizi wa Marekani wa kuendelea kuwepo kijeshi nchini humo kutokana na kutoweka wazi ratiba yake ya kuondoka rasmi unazifanya jitihada za wananchi, serikali na makundi mbalimbali ya Afghanistan za kuhitimisha vita na kurejesha amani ya kudumu nchini mwao zisiwe na athari yoyote.../  

Tags

Maoni