Oct 18, 2020 02:28 UTC
  • Mitazamo ya Trump na Biden kuhusu Iran; madai ya ushindi mkabala na kukiri kwamba Marekani imetengwa

Katika kipindi hiki cha kukaribia uchaguzi wa Rais nchini Marekani tarehe 3 Novemba mwaka huu Rais Donald Trump wa nchi hiyo ambaye ni mgombea wa chama cha Republican na Joe Biden wa chama cha Democratic wamekuwa wakizungumzia kadhia ya Iran na mapatano ya nyuklia ya JCPOA katika kampeni zao za uchaguzi lakini kwa mitazamo tofauti na inayokinzana.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika jimbo la North Carolina, Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine tena amesifu vikwazo vya serikali yake dhidi ya Iran na kudai kuwa mawasiliano ya kwanza watakayopokea baada ya kushinda uchaguzi wa rais yatakuwa kutoka Iran. Trump amehoji akisema: "Je tunaweza kufikia mapatano? Iran inakwenda kuzimu kutokana na vikwazo na hatua zote tulizochukua". 

Hii ni katika hali ambayo akizungumza na televisheni ya ABS, Joe Biden ameshambulia waziwazi msimamo wa Trump kuhusu Iran na taathira zake na kusema: "Marekani hivi sasa imetengwa kuliko wakati mwingine wowote. Iran imekaribia zaidi kumiliki bomu la nyuklia, waitifaki wa Marekani hawana imani na nchi hii na Rais wetu anadhihakiwa katika majukwaa ya kimataifa." 

Joe Biden, mgombea wa kiti cha urais Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrat 

Trump anajigamba kwa matamshi yake ya kuropoka kuhusu alichodai ni mafanikio yake ya kisiasa mkabala na Iran katika frenu ya mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi katika hali ambayo Iran haijakubali takwa lolote haramu na lililo kinyume cha sheria la serikali ya Trump kati ya matakwa yaliyowasilishwa na Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo licha ya kukabiliana na mashinikizo hayo makali yaliyosababishwa na vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa katika historiia. Mwezi Mei mwaka 2018 Pompeo alitaka kusitishwa kikamilifu miradi ya nyuklia ya Iran na kusimishwa miradi ya kutengeneza makombora ya Iran na kuhitimimishwa kile alichokitaja kuwa hatua za Iran katika eneo la Magharibi mwa Asia. Mkabala na mashinikizo yote haya, Tehran imesimama imara, na serikali ya  Trump hivi sasa imetengwa katika uga wa kimataifa. Trump aliahidi kwamba atailazimisha Iran kuuketi kwenye meza ya mazungumzo na Washington ili kufikia eti matapano bora baada ya kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kunzisha mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Tehran. Marekani imegonga mwamba katika jitihada zake za kutekeleza malengo hayo na ndio maana Trump amekosolewa na makundi mbalimbali nchini Marekani  hususan katika kipindi hiki cha kukaribia uchaguzi wa Rais nchini humo.

Sisitizo la Biden, hasimu wa Trump kutoka chama cha Democratic juu ya kushindwa siasa zake mkabala na Iran na kutengwa Marekani hata baina ya waitifaki wake pia linaonyesha kwamba, madai ya Trump dhidi ya Iran hayana mteja hata ndani ya Marekani kwenyewe; na wanasiasa wa nchi hiyo wanakiri kikamilifu kwamba Washington imegonga mwamba na kufeli katika uga wa kimataifa.  

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani  

Kirk Dorsey mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha New Hamsphire anasema: Trump bado anataka kudhihirisha taswira ya hatua zake kali kuhusu Iran. Ni wazi Marekani itarejea katika mapatano ya JCPOA au kukaribia katika kile kinachofanana nayo iwapo Biden ataibuka mshindi katika uchaguzi wa rais.  

Trump anadai kuwa mawasiliano ya kwanza baada ya yeye kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani yatatoka Iran. Pamoja na hayo, tunapasa kumuuliza kwamba, anatoa madai hayo kwa kutegemea ushahidi na uthibitisho upi? Msimamo wa Tehran umejengeka katika muqawama wa kiwango cha juu zaidi mkabala na mashinikizo yasiyo ya kibinadamu na yaliyo kinyume cha sheria ya Marekani.  

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei tarehe 12 mwezi huu wa Oktoba alilsema: Tutaendelea kusimama imara na kufanya muqawama, na kwa baraka za Mwenyezi Mungu tutabadili mashinikizo hayo ya juu zaidi ya Marekani na kuwa fedhehe ya juu zaidi na majuto kwa Marekani. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei 

Ni muhimu kuzingatia jambo hili kwamba mtazamo wa Tehran kuhusu uhasama wa marekani dhidi ya Iran hautofautishi kati ya Warepublican na Wademocrat, na tofauti pekee iliyopo baina ya vyama hivyo viwili ni katika mbinu na namna ya kuamiliana na Iran. Kama ambavyo vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran vilivyotekelezwa kwa kisingizio cha miradi ya nyuklia ya Tehran yenye malengo ya amani vilianza katika utawala wa  Barack Obama rais mstaafu wa Marekani na vingali vinatekelezwa katika utawala wa sasa rais wa nchi hiyo. 

Tags